CCM Singida: Sababu zilizomfanya Lazaro Nyalandu kujiondoa CCM ni kukosa Uwaziri - KULUNZI FIKRA

Tuesday, 31 October 2017

CCM Singida: Sababu zilizomfanya Lazaro Nyalandu kujiondoa CCM ni kukosa Uwaziri

 Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida kimesema sababu zilizotolewa na aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu za kuacha ubunge hazina mashiko, isipokuwa kilichomsukuma kufukia uamuzi huo ni hasira za kukosa uwaziri.

Katibu wa CCM mkoani Singida, Jamson Mhagama alisema jana Jumatatu Oktoba 30,2017 kuwa, “Kwa maono yake ameona siasa za nchi haziendi vizuri na kuamua kwenda kusaka siasa zitakazompendeza, tunamtakia kila la kheri. Ila tunamwonya kuwa asitarajie tena kupata ubunge kupitia Chadema anakolilia kwenda, CCM itashinda kwa kishindo katika uchaguzi mdogo ujao,” alisema Mhagama.

“Wananchi walimwamini Nyalandu katika vipindi vyote vinne kwa kumpa kura za kutosha za nafasi ya ubunge. Kupitia kura hizo, Nyalandu amesifika na kujulikana kila kona sasa ameamua kuwapa kisogo wakazi wa jimbo la Singida Kaskazini, jina lake linaenda kufutika na hatasikika tena,” amesema Mhagama.

Akizungumzia uamuzi wa Nyalandu, mkazi wa Msisi katika Jimbo la Singida Kaskazini, Juma Kindimanda amesema hajawatendea haki wao waliompigia kura kwa kipindi cha takriban miaka 20.

“Kwa kura zetu, Nyalandu ameweza kuaminiwa hadi kupewa nyadhifa za uwaziri katika wizara mbalimbali. Kura hizihizi zimewezesha jina lake kujulikana ndani na nje ya Tanzania. Sasa ameamua kutuacha bila hata kutuheshimu kwa kuja kutangaza uamuzi huo kwenye jimbo lake,” amesema Kindimanda.

Katika hilo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Singida, William Mwang’imba amesema kwa jumla wilaya haina shida na Nyalandu na kwa kuwa ameamua kuondoka, basi aende salama.

Tofauti na kauli hizo za CCM, Chadema Mkoa wa Singida imempongeza Nyalandu kwa uamuzi wake, ikisema milango ipo wazi kwa yeye kujiunga na chama hicho.

Mwenyekiti wa Chadema mkoani Singida, Shaban Limu amesema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, wanapokea mtu yeyote kutoka kokote kuwa mwanachama.

“Alichofanya Nyalandu ni sahihi. Wapo baadhi ya viongozi wakiwemo mawaziri na wabunge hawaridhishwi na hali iliyopo sasa lakini ni waoga, wanaogopa kupoteza masilahi yao,” amesema Limu.

No comments:

Post a Comment

Popular