RC Tabora amwagiza OCD Sikonge kumtamfuta polisi aliyemkejeli mwananchi na DC - KULUNZI FIKRA

Friday, 8 September 2017

RC Tabora amwagiza OCD Sikonge kumtamfuta polisi aliyemkejeli mwananchi na DC

 Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Sikonge ameagizwa kuchunguza tukio Polisi mmoja wilayani humo kumtolea lugha ya kejeli mwananchi akimhusisha na Mkuu wa Wilaya hiyo mapema mwezi Aprili mwaka huu.

Uamuzi huo umetolewa jana mjini Sikonge na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri baada ya Mkazi mmoja wa Sikonge Hidaya Hussein kumweleza kiongozi huyo wakati akisikiliza kero mbalimbali za wananchi.

Hidaya alisema kuwa mnamo Aprili 26 mwaka huu alitoka kwake kwenda kuangalia katika kibanda kuangalia Sherehe za Muungano kwenye runinga na aliporejea alikuta Polisi wamevunja mlango wake na kuingia ndani ya nyumba yake bila ya yeye kuwepo na kupekua bila kuona kitu kibaya.

Alisema kuwa baada ya kukuta tukio hilo aliamua kwenda katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya lakini akiwa njia kuna mtu akamshauri aanzie kwa OCD na ndipo alipofika Polisi na kumkutana Mkuu huyo wa Polisi aliyempangia mtu wa kumsaidia.

Hidaya alisema kuwa wakati akiwa anaendelea na mahojiano ndipo Polisi aliyepangiwa kumsaidia alitoa kauli ya kumkejeli yeye na DC jambo lilimuuma sana kwa sababu alikuwa akidai haki yake.

Mkazi huyo alinukuu baadhi ya maneno aliyomtamkia “Ulitaka kwenda kwa Mkuu wa Wilaya kushitaki …unadhani tunamuogopa Mkuu wa Wilaya…kwanza ujui na wewe tunaweza kukuwekea bangi kisha tukukamate”

Hidaya alisema kuwa nia yake ya kwenda Polisi ilikuwa ni kutaka kujua kwanini waliendesha upekuzi wakati hayupo na kama walihisi kuna shida wangeweza kuwatuma watoto wamfuate alipo.

Alisema kauli hiyo ilimuuma sana na baada ya kusikia Mkuu wa Mkoa wa Tabora anakuja kuwasilikiza akamua kwenda kufikishia kilio chake.

Akijibu hoja hiyo Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amemuagiza Mkuu wa Polisi Wilaya kumtafuta Polisi aliyetoa lugha hiyo na kumchukulia hatua na kuongeza kuwa kwa sababu mwananchi anamjua mhusika gwaride la utambuzi lifanyike.

Alisema kuwa hawezi kuacha tabia hiyo iendelee kwani mtumishi kama ameonyesha dharua kwa Mkuu wa Wilaya ni sehemu ya kuelekea kumdharua yeye(RC).

“Kama askari huyo au hawa wametoa lugha hiyo ya kumdharau Mkuu wa Wilaya , hiyo ni njia ya kuelekea kunidharau mimi … siwezi kukubali ni lazima askari hao watafutwe na wachukuliwe hatua,” alisema Mwanri.

Aidha alisema kuwa alimwagiza OCD kuhakikisha Hidaya na wananchi waliojitokeza kueleza kero wanazofanyiwa na baadhi ya watumishi walindwe.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Peres Magiri alisema hawezi kuvumilia kuona kuna watumishi watoa matamshi yanayonyesha dharua kwake na kwa wananchi.

Alisema kuwa watakaobaika atamuchukulia hatua ikiwa ni pamoja na kumuondoa katika wilaya anayoingoza mwenyewe.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora baada ya kumaliza zoezi la kusikiliza kero za wakazi wa Sikonge anatarajia kuendelea na Wilaya nyingine.

No comments:

Post a Comment

Popular