Mwandishi wa Safu ya Siasa, Padri Privatus Karugendo, anashauri siasa zinazofanyika nchini zifuate utandawazi wenye ubinadamu kwa kuwa demokrasia Tanzania bado ni kitendawili.
Anasema, “Mtu kuwa kwenye chama cha upinzani ni kama kufanya dhambi ya mauti. Nimesikia kwamba kuna baadhi ya viongozi wa dini wanaofundisha kwamba upinzani wa kisiasa ni dhambi.
“Wanawalinganisha wapinzani wa kisiasa na wapinzani waliokuwa wakijitokeza kwenye dini zao katika historia. Tumeshuhudia vituko vingi wanavyofanyiwa watu waliojitenga na CCM na kujiunga na vyama vya upinzani, hadi wanapiga magoti kuomba msamaha wa kurudishwa ndani ya kundi.”
Karugendo anaongeza, “Wakati tunayashinikiza mashirika ya kimataifa kubadilisha mifumo yake na kuyataka kutuletea utandawazi wenye sura ya ubinadamu, ni lazima na sisi tuanze kubadilika. Tujifunze kuwajibika, tujifunze kuwa wazi, tujifunze kusema ukweli, tujifunze kulitanguliza taifa letu kuliko kutanguliza sifa, tamaa na maslahi binafsi.
“Ni lazima sisi pia tuonyeshe utayari wa kupokea utandawazi wenye sura ya ubinadamu. Vinginevyo tunajiingiza kwenye utumwa, na utumwa daima hauna sura ya ubinadamu.
“Tunapompongeza Rais wetu Magufuli, kwa kazi kubwa anayoifanya. Ni muhimu pia kumkumbusha dunia yetu. Ni muhimu kutambua kwamba pamoja na mabadiliko tunayoyafanya kama taifa, hatuwezi kuishi nje ya dunia hii ya utandawazi. Tuwe wapole kama njiwa, lakini wajanja kama nyoka. Ni muhimu kujenga taifa imara ndani ya utandawazi wenye sura ya ubinadamu. Utandawazi unaolinda uhai na heshima ya kila Mtanzania.
No comments:
Post a Comment