Msukuma: RPC Mponjoli kushindwa kuniomba radhi, sasa nitaweka hadharani madudu yote anayoyafanya - KULUNZI FIKRA

Friday, 29 September 2017

Msukuma: RPC Mponjoli kushindwa kuniomba radhi, sasa nitaweka hadharani madudu yote anayoyafanya

 
 Akizungumza na kulunzifikra blog  jana, Musukuma alisema baada ya muda aliokuwa ametoa kwa kamanda huyo kuomba radhi kupita, ataweka hadharani madudu yote yanayofanywa na RPC huyo wiki ijayo atakapokuwa amerejea mkoani humo akitokea Zanzibar aliko kwa sasa.

 "Niko Zanzibar naumwa na kwa leo (jana) sitaweza kulizungumza kwa kina hilo suala," alisema Musukuma ambaye ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita na ambaye alikaa mahabusu kwa siku tatu kabla ya kufikishwa mahakamani Septemba 19.

  Musukuma na wenzake nane wanakabiliwa na mashtaka manne ya jinai, likiwamo la kula njama.

 "Nikirudi (Geita) tu nitaitisha mkutano na waandishi wa habari na kuweka hadharani yale niliyokuwa nimeyaahidi nilipozungumza wiki iliyopita."

 Wiki iliyopita, Musukuma alimpa siku nne Mponjoli kumwomba radhi la sivyo ataweka hadharani alizodai kashfa zake, ikiwamo madai ya kujilimbikizia mali.

 Musukuma alilalamikia hatua ya RPC huyo kumkamata katika mazingira aliyoita ya kumdhalilisha kwa kumshika suruali nyuma kama mhalifu, wakati yeye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Geita na mwakilishi wa wananchi.

    Alisema RPC huyo asipoomba radhi ataanika hadharani alichoita maovu yake, ili vyombo vya uchunguzi kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), vianze kuchunguza.

    Musukuma alimlaumu Kamanda huyo kwa kumkamata na kumweka mahabusu wakati angeweza kumwita na kuzungumza naye kwa staha kwa kuwa yeye ni kiongozi wa chama na mwakilishi wa wananchi.

"Tangu CCM iundwe mwaka 1977 mimi nimeweka rekodi ya kuwa Mwenyekiti wa kwanza kuwekwa ndani na RPC wangu," alisema zaidi Musukuma na kulalamika zaidi:

 "Nakwambia RPC kwa kuwa umenichokoza, na kwa kuwa umeamua kuingia kwenye hii ligi, basi jiandae. Umeliamsha dude na mimi nitaliamsha kwelikweli." Alisema kama Mponjoli anataka amani atafute wazee wanaomheshimu kama Mwenyekiti wa CCM na kwenda kuzungumza.

 Aliwataka wakazi wa Geita kukaa mkao wa kusikiliza sababu za yeye kukamatwa na RPC huyo na kwamba vitu vyote ambavyo RPC huyo amewekeza mkoa wa Geita na mengine angetaja baada ya siku hizo. Amekuwa kimya hata hivyo.

 Alipotafutwa kwa njia ya simu kupata maoni yake juu ya kauli hiyo ya Musukuma jana, Kamanda Mponjoli alisema yeye anazungumzia masuala ya jinai tu.

 "Mkiniuliza mambo ya uhalifu nitawaambia, lakini hayo mambo anayosema Mbunge siwezi kuyazungumzia," alisema RPC Mponjoli.

   
    

No comments:

Post a Comment

Popular