Mbunge wa CCM amtembelea Tundu Lissu hospitalini kumjulia hali jijini Nairobi - KULUNZI FIKRA

Saturday, 16 September 2017

Mbunge wa CCM amtembelea Tundu Lissu hospitalini kumjulia hali jijini Nairobi

   Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Mhe. Lazaro Samuel Nyalandu amemtembelea Mbunge wa Singida Mashariki Mhe. Tundu Lissu jijini Nairobi nchini Kenya kumjulia hali kufuatia mbunge huyo kupigwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7,2017 akiwa mjini Dodoma.

Lazaro Nyalandu amesema kuwa kwa niaba ya watu wa Singida na Watanzania wote ametoa salamu za pole kwa mke wa Tundu Lissu kwa kuwa bado hajapata nafasi ya kumuona kiongozi huyo na kusema anasubiri kama ataweza kupata nafasi ya kumuona usiku wa leo kama madaktari wataruhusu.

"Nimefika hospitali ya Nairobi mapema leo kumjulia hali Mhe. Tundu Lissu madaktari wanaendelea kumfanyia matibabu, na bado hatujaruhusiwa kumuona. Kwa niaba ya wana Singida na Watanzania wote, nimetoa salamu za pole kwa mke wake, na bado nasubiri uwezekano wa kuweza kuonana naye usiku wa leo endapo madaktari wataruhusu", alisema Nyalandu.

Aidha Mbunge huyo amewataka Watanzania kiujumla kuendelea kumuombea Mbunge Tundu Lissu ili aweze kupona na kurejea nchini akiwa mzima wa afya njema.

"Cha muhimu zaidi, sote tuendelea kumuombea Mungu amtendee wema, na kumponya katika majira haya ya kujaribiwa kwake. Katika yote ndani ya yote, ikiwa heri kwake", alisema Nyalandu.

Mbunge Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7,2017 akiwa Makao Makuu ya nchi mjini Dodoma na baadaye kupelekwa jijini Nairobi Kenya kwa matibabu ambapo mpaka sasa yupo huko akiendelea kupata matibabu.

No comments:

Post a Comment

Popular