Iringa: Jeshi la polisi lamshikilia mwalimu kwa kumchapa mwanafunzi na kusababisha kifo - KULUNZI FIKRA

Monday 4 September 2017

Iringa: Jeshi la polisi lamshikilia mwalimu kwa kumchapa mwanafunzi na kusababisha kifo

JESHI la Polisi mkoani Iringa linamshikilia Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi, Ng’ingula, Wilaya ya Kilolo, Robson Sanga (59), kwa tuhuma za kumua mwanafunzi wa darasa la tano, Emmanuel Gavile (13) kwa kumchapa fimbo mapajani kwa kuchelewa shuleni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi, alisema tukio hilo lilitokea Agosti 16, mwaka huu saa 3.00 asubuhi shuleni hapo baada ya mwanafunzi huyo kudaiwa kuchelewa kufika shuleni kwa muda ambao shule imeuweka.

Alisema kutokana na adhabu hiyo, Gavile alilia kwa maumivu makali na kushindwa kujisomea hali iliyowafanya wenzake kumkimbiza katika zahanati ya kijiji hicho ambako hali ilizidi kuwa mbaya.

Baadaye alihamishiwa Kituo cha Afya Usokomi wilayani humo.

“Agosti 26 mwaka huu mwanafunzi huyo alihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa akilalamikia maumivu makali katika paja la mguu wa kulia kabla ya kufariki dunia saa 3.00 asubuhi,” alisema Mjengi.

Kamanda alisema uchunguzi wa daktari umeonyesha kuwa kifo cha mwanafunzi huyo kilisababishwa na kupasuka mfupa wa paja la mguu wa kulia na damu kuviria katika mapafu yake.

Alisema kwa muda wote huo wazazi hawakuweza kuripoti polisi ila baada ya kifo cha mwanafunzi huyo ndipo walipofika kituo cha polisi kutoa taarifa na jeshi hilo limemkamata mwalimu huyo kwa uchunguzi.

No comments:

Post a Comment

Popular