Abiri wasababisha ndege kuchelewa kupaa baada ya kusema " Allah Akbar" - KULUNZI FIKRA

Monday 4 September 2017

Abiri wasababisha ndege kuchelewa kupaa baada ya kusema " Allah Akbar"

 Abiria tisa wamezua taharuki kwenye kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Zaventem, nchini Ubelgiji baada ya mmoja wao kutamka matamshi yaliyosikika ‘Allah Akbar’ kwa sauti kubwa mara kadhaa.

Watu hao tisa walitolewa na maaskari kwenye ndege ya shirika la Ryanair, na kuamriwa mizigo yao kutolewa kwenye ndege ili kukaguliwa zikiwa zimebakia dakika 10 kabla ya ndegehiyo kuondoka.

Ndege hiyo ililazimika kuchelewa kwa masaa manne ikipisha ukaguzi wa mizigo ya watu hao, ambao walitambuliwa kuwa ni raia wa Ubelgiji.

Polisi mjini Brussels wamethibitisha taarifa hizo kupitia kituo cha Runinga cha VTM  news kwa kusema kuwa ni kweli tukio hilo limetokea siku ya Jumamosi Tarehe 2 Septemba ambapo wavulana hao tisa walikuwa wanasafiri kutoka Mjini Brussels kwenda Madrid, Hispania.

“Tumepokea taarifa hizo za wanaume tisa waliokuwa wakisafiri kutoka Ubelgiji kwenda Madrid, Hispania lakini walipoingia kwenye ndege mmoja wao akaanza kutamka kwa sauti ‘Allah Akbar’ akimaanisha ‘Mungu mkubwa’ kama mara sita hivi ndipo askari wa usalama wakamtoa kwenye ndege pamoja na wenzake wote kwa ukaguzi”,amesema Peter De Waele msemaji wa jeshi la Polisi mjini Brussels .

Kwa mujibu wa taarifa kutoka gazeti la Top 24 abiria walioshuhudia tukio hilo wamesema lilitokea baada ya ndege hiyo kuchelewa masaa matatu kuruka na ndipo mtu huyo akaanza utani akitamka ‘Allah Akbar’ huku akicheka.

Hata hivyo abiria hao nane walirudishwa kwenye ndege baada ya ukaguzi kufanyika na ndege kuendelea na safari yake, ingawaje mpaka sasa bado haijawekwa wazi sababu za kupekuliwa kwa watu hao kwa mara ya mbili huku mitandao mingi duniani ikiandika kuwa ni hofu ya ugaidi iliyotanda nchini Ubelgiji.

No comments:

Post a Comment

Popular