Sheikh Mkoa wa Dar es salaam ataka waliokwamisha mahujaji wakamatwe - KULUNZI FIKRA

Sunday 27 August 2017

Sheikh Mkoa wa Dar es salaam ataka waliokwamisha mahujaji wakamatwe

 
 Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum amesema taasisi iliyokusanya fedha kwa waumini wapatao 100 na kushindwa kuwasafirisha kwenda hija, isakwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Tangu Agosti 23, waumini hao wamekwama Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere baada ya taasisi hiyo (jina linahifadhiwa kwa sasa) kuchukua hadi Sh10 milioni kutoka kwa kila hujaji, lakini ikashindwa kufanikisha safari hiyo.

Sheikh Salum alisema jana kuwa kuna haja kwa wahusika wa taasisi hiyo kusakwa, kukamatwa na kushtakiwa mahakamani kwa kuwa licha ya kuwatapeli mahujaji hao, imesababisha washindwe kutimiza azma yao ya kufanya ibada hiyo.

“Zipo taasisi zenye tabia ya kuwatapeli waumini na hii si mara ya kwanza. Niwape faraja mahujaji waliokwama kwamba kama mwaka huu hawajasafiri labda Mwenyezi Mungu alipanga wasafiri mwaka ujao. Cha msingi ni kuwa makini na kampuni za aina hii,” alisema.

“Kuna waumini wengine wamezuiwa kuingia Saudi Arabia kwa sababu taasisi zilizowasafirisha nazo hazina vibali vya kuingia huko. Sasa ni kwa nini wasafirishe watu wakati wanajua wazi kwamba hawajatimiza vigezo?”

Baadhi ya waumini waliokwama kusafiri wameiomba Serikali kuingilia kati ili warejeshewe fedha zao. Walisema mpaka jana jioni hawakuwa na taarifa zozote kuhusu safari yao, wakati fedha zote walishailipa taasisi hiyo yenye ofisi zake Kariakoo jijini hapa.

Mmoja wa watu waliokuwa wasafiri, Ummy Sekibo alisema licha ya jitihada za kutoa taarifa kwenye taasisi za kidini, vyombo vya habari na Jeshi la Polisi bado wameshindwa kuondoka.

“Hakuna matumaini tena kama taasisi hii inaweza kutusafirisha, maana tangu Agosti 23 tumeganda hapa na hatujui tufanye nini,” alisema Sekibo.
Ummy alisema kwa sababu lengo lake lilikuwa ni ibada, ameanza mchakato wa kutafuta fedha nyingine haraka ili aweze kusafiri huku akiendelea kushughulikia fedha zake ‘alizotapeliwa.

Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Rajab Tendwa, alisema kila muumini amelipa fedha kulingana na makubaliano na taasisi hiyo. Walilipa kati ya Sh8.5 milioni hadi Sh10 milioni.

No comments:

Post a Comment

Popular