MwanaFA, AY wazidi kuibana koo tigo mahakamani - KULUNZI FIKRA

Friday 25 August 2017

MwanaFA, AY wazidi kuibana koo tigo mahakamani

 
 Dar es Salaam. Wasanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya nchini, Hamisi Mwinyijuma maarufu kwa jina la MwanaFA na Ambwene Yesaya maarufu kama AY wamezidi kuikaba koo kampuni ya huduma za simu za mkononi ya Tigo mahakamani, baada ya kuiwekea pingamizi katika maombi yake.

Tigo ilifungua maombi katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, wakiiomba iiongeze kampuni ya Cellulant Tanzania Limited, kama mmoja wa wadaiwa, kwenye hukumu ya Mahakama hiyo iliyoiamuru Tigo kuwalipa wasanii hao fidia ya Sh2.1 bilioni.

Katika hukumu yake iliyotolewa Aprili 11, 2016, Mahakama hiyo iliiamuru Tigo kuwalipa wasanii hao fidia ya kiasi hicho cha fedha kwa kosa la kukiuka Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki, kwa kutumia kazi zao kama miito ya simu bila ridhaa wala makubaliano nao.

Kazi hizo ambazo kampuni hiyo ilizitumia bila ridhaa wala makubaliano ni wimbo uitwao ‘Usije Mjini’ wa MwanaFA na ‘Dakika Moja’ wa AY.

Hata hivyo, Tigo imewasilisha maombi ikiomba kuongezwa kwa kampuni ya Cellulant kwenye hukumu hiyo, kwa madai kuwa ndiyo iliyoipelekea nyimbo za wasanii hao. Wakili wa Tigo, Rosan Mbwambo alisema mteja wake aliingia makubaliano na kampuni hiyo iwaletee nyimbo na haikujua kama haikuwa na makubaliano na wahusika, lakini mahakama katika hukumu yake haikuihusisha kampuni hiyo.

Hata hivyo, wasanii hao kupitia kwa wakili Albert Msando wameyawekea pingamizi maombi hayo ya Tigo, wakiiomba mahakama hiyo iyatupile mbali.

Pingamizi hilo lilikuwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ritha Tarimo jana na baada ya kusikiliza hoja za pande zote alipanga kutoa uamuzi Agosti 31.

No comments:

Post a Comment

Popular