Katika kuhakikisha wanafikia malengo yao, Klabu ya Simba SC imewataka wanachama wake kujitokeza kwa wingi katika mkutano mkuu wa mwaka utakaofanyika leo kuanzia saa 4:00 asubuhi kwenye Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere.
Kaimu Makamu wa Rais wa Simba, Idd Kajuna, awali aliwahakikishia mwandishi wetu kuwepo kwa mkutano huo ambao licha ya malengo yake kuweka wazi, ni unaelezwa ni kwenda kupitisha uamuzi wa kumuuzia hisa mfadhili wa klabu hiyo Mohammed Dewji 'MO' awe mmiliki rasmi wa Simba.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara alinukuliwa jijini Dar es salaam jana akisema mkutano wa Jumapili (leo) upo pale pale kufuatia mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es salaam kutupilia mbali ombi la mmoja wa wadhamini wa klabu hiyo, Hamisi Kilomoni kuzuia usifanyike.
"Tunawaomba wanachama kuhudhuria kwa wingi mkutano huo muhimu mahitaji yote yatapatika ikiwemo chakula na vinywaji".
"Uamuzi wa Mahakama ni ushindi mkubwa siyo tu kwa klabu, bali kwa mustakabali mzima wa maendeleo ya mchezo wa soka nchini", alisema Manara
MO anataka kuuziwa asilimia 51 ya hisa za klabu kwa Shs bilioni 20 na baada ya hapo atatumia bajeti ya Shs bilioni 5.5 kwa msimu kwa ajili ya Simba SC, ili kuifanya klabu hiyo kuwa ya kisasa ikiwemo kuujenga Uwanja wa Bunju.

No comments:
Post a Comment