PIKIPIKI 14 aina ya Vespa zenye thamani ya Sh milioni 37, zimetolewa na Mbunge wa Jimbo la Kiwengwa, Khamis Mtumwa kwa makatibu wa matawi ya CCM ya jimbo hilo.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vitendea kazi hivyo huko kwenye Uwanja wa Mpira wa Kwa Gube, mbunge huyo alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo.
Alieleza kwamba lengo la kutoa vifaa hivyo ni kuwarahisishia huduma za usafiri watendaji hao ambao muda mwingi wanakuwa na majukumu mbalimbali yanayohitaji usafiri wa haraka ili yatekelezwe kwa wakati.
Aliahidi kuwa hiyo ni sehemu tu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jimbo hivyo ataendelea kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo. “Nitaendelea kumarisha huduma mbalimbali za kijamiii kadri Mwenyezi Mungu atakavyonijaalia, wito wangu kwenu ni kwamba miradi ambayo kwa sasa naitekeleza katika jimbo hili mnatakiwa kuitunza ili iweze kuwanufaisha watu wote,” alisisitiza Mtumwa.
Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ baada ya kukabidhi pikipiki hizo kwa watendaji hao, aliwataka viongozi wa majimbo ya chama hicho kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi. Alisema kwa sasa viongozi wanatakiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo ili wananchi waone maendeleo.
No comments:
Post a Comment