Kesi za rushwa zamkera Rais Magufuli - KULUNZI FIKRA

Thursday 24 August 2017

Kesi za rushwa zamkera Rais Magufuli

Rais John Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na taratibu za uchunguzi na uendeshaji wa mashitaka ya rushwa zinavyochukua muda mrefu na ametoa wito kwa viongozi wa TAKUKURU kufanyia kazi vita dhidi ya rushwa na ionekane ikizaa matunda haraka.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo mara baada ya kumuapisha Brigedia Jenerali John Julius Mbungo kuwa naibu mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ikulu jijini Dar es Salaam

“Tukifanikiwa kupunguza rushwa kwa angalau asilimia 80, nchi yetu itafanikiwa kutatua matatizo mengi, na ni vyema mtambue kuwa hatua hizi tunazochukua zimeanza kuwavutia wafadhili wengi na wawekezaji. Na mimi nikiwa kiongozi wenu nimeamua kupambana na rushwa kikwelikweli, na ninawaomba nyote mshirikiane kuondoa rushwa katika maeneo yenu ya kazi” amefafanua Rais Magufuli.

Pia rais Magufuli amewataka viongozi wote nchini kushirikiana katika jukumu la mapambano dhidi ya rushwa ili kuepusha madhara ya tatizo hilo katika uchumi na ustawi wa jamii.

“Ukiangalia mambo makubwa tunayopambana nayo yanasababishwa na rushwa iliyosambaa kila mahali, watumishi hewa chanzo ni rushwa, dawa za kulevya ndani yake kuna rushwa, vyeti feki ndani kuna rushwa, mikataba mibovu ndani kuna rushwa, pembejeo za ruzuku ndani kuna rushwa na huko mahakamani nako ni rushwa tu,” amesisitiza Rais Magufuli.

Ameipongeza TAKUKURU kwa kazi iliyoanza kuifanya lakini ametaka juhudi zaidi ziongezwe ili watu wote wanaojihusisha na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.

Naye Brigedia Jenerali Mbungo baada ya kuapa, ameshukuru kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo na ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wengine wa TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa.

No comments:

Post a Comment

Popular