Mwenyekiti wa IEBC amemtangaza Rais Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais
Bw Kenyatta alipata kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27 ya kura zilizopigwa
Bw Raila Odinga alipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74 ya kura zote zilizopigwa
Waliojitokeza walikuwa 15,073,662 ambayo ni asilimia 78.91 kati ya 19m waliokuwa wamejiandikisha kupiga kura
Upinzani ulidai Alhamisi kwamba Raila Odinga alishinda uchaguzi na kuitaka tume imtangaze kuwa mshindi wa urais
Kura zilizoharibika zimeendelea kuwa nyingi, na kufikia sasa ni kura 399 935.
Habari za moja kwa moja
Kenyatta: Nawashukuru wananchi kwa kuwa na imani nami
Imepakiwa mnamo
22:23
Rais Kenyatta, akihutubu baada ya kutangaza mshindi wa urais amewashukuru wananchi kwa kuwa na imani naye na serikali yake.
"Nawaahidi tutaendelea na kazi tuliyoianza. Nawashukuru sana Kenya. Kadhalika, naishukuru tume ya uchaguzi kwa kazi nzuri waliyoifanya," amesema.
"Nawapongeza wote walioshinda, na kwa walioshindwa pia tutaishi kupambana siku nyingine."
Kwa upinzani amesema: "Sisi si maadui, ni raia wa nchi moja. Kila shindano, kutakuwa na washindi na wanaoshindwa, lakini tutasalia kuwa Wakenya. Nawapa moyo wa ushirikiano, twafaa kuungana pamoja. Wakenya wanataka sisi tufaulu."
"Sana kwa Raila Odinga, namuomba yeye, wafuasi wake, wote waliochaguliwa kupitia upinzani, tutafanya kazi pamoja, tutashirikiana, tutakua pamoja na kuendeleza nchi pamoja."
"Kwa Wakenya wenzangu, uchaguzi huja na kuondoka lakini Kenya itaendelea kuwepo, tukumbuke daima kwamba sisi ni ndugu na dada. Jirani yako bado ni jirani yako. Tuendelee kudumisha amani. Hakuna haja ya fujo, sisi wanasiasa pia huja na kuondoka. Lakini jirani yako atabaki."
"Mengi zaidi tutasema kesho."

No comments:
Post a Comment