Rais John Magufuli ameendelea kusisitiza msimamo wake wa kuwataka wawekezaji walioshindwa kuviendeleza viwanda walivyobinafsishwa kuvirejesha, huku akimtaja mbunge wa Morogoro mjini (Abdulaziz Abood) kuwa miongoni mwa wanaopaswa kutekeleza agizo hilo.
Dkt. Magufuli amesema hayo Leo Alhamis Julai 27, Morogoro mjini, akiwa njiani kurejea Dar es Salaam, akitokea mikoa ya Kigoma, Tabora na Singida, ambako alifanya mikutano mbalimbali ikiwemo ya uzinduzi wa miradi ya maendeleo.
“Narudia wito wangu niliokwisha kuutoa hapo nyuma, kwamba wenye viwanda wa Morogoro ambao wameshindwa kuviendesha hivi viwanda, na leo nataja akiwepo mbunge wa hapa wa CCM, narudia akiwepo mbunge wa hapa wa CCM, ambaye alibinafsishwa viwanda vingi ambavyo sasa vinafugiwa mbuzi, kama ameshindwa kuviendesha avirudishe,” amesema Magufuli.
Tangazo hilo la kiongozi huyo mkuu wa nchi, lilipokelewa kwa shangwe na nderemo na wananchi waliokuwa wakimsikiliza rais akiwa amesimama juu ya gari lililombeba, baada ya kumsimamisha.
Rais ametanabaisha kuwa lengo la kurejeshwa kwa viwanda hivyo ni kutaka kupewa watu wengine ambao wataweza kuviendeleza, kwani kusimama kwake kunafanya vijana wengi kukosa ajira.
Kwa mujibu wa mwandishi wa Azam TV, Robert Mayungu aliyopo mkoani Morogoro, mbunge huyo anamiliki viwanda vitatu, kikiwemo kiwanda cha sabuni cha komoa, japo inatajwa kuwa moja ya viwanda hivyo tayari kimeanza kuimarika.
No comments:
Post a Comment