Vigogo Takukuru, Jeshi la polisi na Elimu wajitosa kutekeleza Agizo la Rais Magufuli. - KULUNZI FIKRA

Friday 4 May 2018

Vigogo Takukuru, Jeshi la polisi na Elimu wajitosa kutekeleza Agizo la Rais Magufuli.

 
Siku moja baada ya Rais John Magufuli kuviagiza vyombo vya dola kuwachukulia hatua waliohusika na ujenzi wa jengo la ukumbi wa Chuo Kikuu cha Elimu Mkwawa (Muce), uchunguzi umeanza.

Juzi, akizungumza na wafanyakazi na wanafunzi wa Muce mjini Iringa, Rais Magufuli aliagiza vyombo hivyo ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kufuatilia ujenzi huo uliogharimu Sh8 bilioni.

Rais Magufuli alisema hayo baada ya wanafunzi wa Muce kumuomba wajengewe mabweni ili wawe karibu na chuo hicho, jambo alilosema haliwezekani kwa sasa hadi aone matokeo ya fedha za Serikali katika ujenzi wa ukumbi.

“Naviomba vyombo vya dola ikiwamo Takukuru na polisi kufuatilia suala hili, mkishindwa nitafuatilia mwenyewe,” alisema Rais Magufuli katika mkutano huo.

Walipotafutwa kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa Takukuru, Jeshi la Polisi na Wizara ya Elimu walisema kilichosemwa na Rais ni agizo, hivyo hawana budi kulitekeleza mara moja.

“Haya ni maagizo, hatuwezi kurudi nyuma lazima tufuatilie. Tumeshaanza uchunguzi kwa kufuata utaratibu na kanuni, lakini kwa sasa siwezi kusema tumefikia wapi kwa sababu agizo lilitolewa jana (juzi),” alisema naibu mkurugenzi wa Takukuru John Mbungo.

Alisema bado ni mapema kutoa taarifa, lakini chochote kinachoagizwa na Rais huwa wanaanza utekelezaji mara moja.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo alisema wameshaanza kuyafanyia kazi maelekezo ya Rais Magufuli kwa mujibu wa taratibu na kanuni.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema maelekezo yanayotolewa na Rais huwa hayajadiliwi, bali yanatekelezwa na ndicho kinachofanyika sasa.

“Bado hatujampata, tukimpata tutawaeleza. Yale ni maelekezo huwa hatujadili mara mbili, bali tunayatekeleza mhusika akipatikana mtajua tu,” alisema Kamanda Mambosasa akizungumzia agizo la Rais kuwa aliyewahi kuwa mkuu wa chuo hicho, Profesa Philemon Mushi ahojiwe.

Rais Magufuli akiwa Muce alieleza sababu za kukataa kuweka jiwe la msingi la jengo hilo kuwa ilitokana na kujengwa kifisadi.

No comments:

Post a Comment

Popular