Maalim Seif ahidi kuendeleza Demokrasia Nchini. - KULUNZI FIKRA

Wednesday 9 May 2018

Maalim Seif ahidi kuendeleza Demokrasia Nchini.

 
Katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema uimarishwaji wa demokrasia katika vyama vya siasa, ni miongoni mwa sababu za kupiga hatua zaidi za maendeleo.

Maalim Seif alisema hayo katika mazungumzo na mkurugenzi wa taasisi ya International Republican Insitute (IRI), Peter Alingo yaliyofanyika makao makuu ya chama hicho Mtendeni mjini Unguja.

Alingo alikwenda kujitambulisha kama kiongozi mpya wa taasisi hiyo baada ya mtangulizi wake kustaafu. makao makuu ya taasisi hiyo yapo nchini Marekani.

Maalim Seif alisema CUF kikiwa chama cha siasa kitahakikisha kinaendelea kuhubiri na kusimamia demokrasia kwa kuwa kinaamini uwapo wake, ndiyo chachu ya mabadiliko ya utendaji ndani ya chama hicho na Taifa.

Alisema wakiwa wadau wa haki na usawa watahakikisha wanamuunga mkono kiongozi huyo mpya wa taasisi hiyo na wengine wenye malengo ya kusimamia demokrasia na kuhubiri amani.

“CUF siku zote inaamini katika demokrasia ndiyo maana tumekuwa na marafiki wengi kutoka asasi tofauti za kimataifa, tutaendelea kuwa tayari kumkaribisha yeyote atakayetaka kushirikiana na sisi,’’ alisema Maalim Seif.

Alieleza kusikitishwa na kile alichokiita kuminywa demokrasia nchini, ikiwamo vyama vya siasa kuzuiwa kufanya mikutano.

Naye Alingo aliahidi kushirikiana na CUF na kwamba, bila uwapo wa amani, hakuna kitu kitakachofanyika katika vyama vya siasa na Taifa.

No comments:

Post a Comment

Popular