Waziri mkuu awaonya viongozi wa Dini Nchini. - KULUNZI FIKRA

Sunday, 1 April 2018

Waziri mkuu awaonya viongozi wa Dini Nchini.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini kutojiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa amani na kusisitiza kuwa serikali haitasita au kufumbia macho wenye kuvunja amani ya nchi.

amelitaka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kuunga mkono juhudi za serikali katika kufikia uchumi wa viwanda kwa kuwekeza kwenye viwanda na majengo na huku akitaka uwepo udhibiti wa taasisi za kitapeli zinaowatapeli Watanzania wanaotaka kwenda hija.

Akizungumza wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa Taifa wa Bakwata jana mjini hapa, Majaliwa alisena serikali inatambua kuwa dini ni kiongozi wa amani, lakini aliwaonya viongozi hao wajiingize kwenye vitendo vya uvunjifu wa amani.

“Kuna vitendo kama vitaruhusiwa kwenye misikiti, madrasa na katika jamii zetu nina hakika vitendo hivyo vitasababisha vurugu, hivyo ni wajibu wetu kuwa vitendo hivyo hatuvipi nafasi katika maeneo yetu. Lakini wale wote wanaoeneza na kusambaza vitendo hivyo tunatakiwa tuwakemee na ikiwezekana tuwaripoti katika mamlaka zinazohusika ili hatua kali dhidi yao zichukuliwe,” amesema Waziri Mkuu.

“Tusiruhusu hata mara moja madrasa zetu, misikiti yetu kuwa viwanda vya kuzalisha chuki na uadui. Hii ni taasisi muhimu katika maisha yetu na ndio maana serikali yetu inaheshimu dini zote kwa sababu ina mchango wake katika amani.”amesema Waziri mkuu.

Aidha, Waziri mkuu  alikemea tabia ya waumini wa Kiislamu kuwa na migogoro ya kugombea misikiti na madaraka na kutaka mkutano huo uende kumaliza matatizo hayo.

“Migogoro mingine ya kutengeneza haina tija, viongozi hubirini neno la Mungu kwa kutumia misahafu na Biblia.. serikali haitasita wala kufumbia macho wanaoleta uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi.”amesema Waziri mkuu.

Waziri mkuu alisema lengo la serikali ni kupigania na kupambania amani ya nchi.

“Serikali na nyinyi pia mnatambua kuwa kuna watu wasioitakia mema nchi yetu na wamekuwa wakifanya kila njia kuhakikisha amani ya nchi yetu inatoweka watu hawa wasipewe nafasi. Amani ni miongoni mwa neema ambayo Mungu ametupa,” amesema Waziri mkuu.

“Niwasihi kuongoza hilo kwa kutumia misahafu na Biblia mkiwa madhabahuni, na kama mnahitaji kutamka yaliyo nje ya vitabu vya Mungu basi yatafutiwe mahala pake. Kwa hiyo tusitafute namna yoyote ya kuchafua amani. Mahubiri yenu yasiwaingize watu jehanamu bali wapelekeni palipo pema.”amesema Waziri mkuu.

Mbali ya kuitaka Bakwata kuunga mkono juhudi za kufikisha nchi katika uchumi wa kati kwa kuwekeza kwenye viwanda na majengo, aliitaka kuzichukulia hatua kali taasisi zinazofanya kazi ya kusafirisha mahujaji, lakini zimekuwa zikiwatapeli.

Ameitaka kuzidhibiti na kuhakikisha fedha za wananchi waliotapeliwa zinarudishwa. Kuhusu suala la tume iliyoundwa kuangalia mali za Waislamu,alisema imeshakabidhi taarifa kwa Rais John Magufuli ili kupitia vyombo vyake na kuhakiki mali hizo na kuwa kwa sasa rais anaendelea na uratibu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,  Mhe Selemani Jafo aliwataka viongozi wa dini kote nchini kushiriki katika kusimama rasilimali fedha ambazo zimetolewa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya huduma na maendeleo.

Mufiti Mkuu wa Tanzania, Shehe Mkuu Abubakary Zuberi alisema katika kipindi chake cha uongozi wamejenga umoja miongoni mwa Waislamu na kukuza mahusiano baina ya madhehebu mbalimbali ya Kiislamu yaliyoko nchini na wale walio nje ya nchi sambamba na kuendesha miradi mbalimbali.

“Kama kuna mtu atasema hakuna jambo lililofanyika labda Mungu amekujalia upofu wa kutoona, lakini Bakatwa imekuwa ikifanya kazi nyingi kuanzia kata, wilaya mkoa hadi Taifa,” alisema Mufti Zubery na kumpongeza Rais Magufuli kusaidia Waislamu kwa kuchagiza ujenzi wa msikiti wa kimataifa utakaokuwa na huduma mbalimbali unaojengwa kwa msaada wa Morocco huku akielezea mpango wa kujenga chuo kikuu.

No comments:

Post a Comment

Popular