Wabunge sita wanusurika kifo katika ajali ya Gari. - KULUNZI FIKRA

Friday, 30 March 2018

Wabunge sita wanusurika kifo katika ajali ya Gari.

 
Wabunge sita wa Jamhuri Muungano wa Tanzania kutoka Visiwani Zanzibar wamenusurika kufa baada ya gari waliyokuwa wakisafiria kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam kupata ajali katika eneo la Bwawani mkoani Morogoro, usiku wa kuamkia leo.

Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro Ulrich Matei, wakati alipokuwa anazungumza na mwandishi wa habari hii na kusema chanzo cha ajali hiyo imesababishwa na mnyama aina ya mbwa aliyekuwa anavuka barabara kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine.

"Ni kweli hili tukio limetokea na muda huu tupo katika kiwanja cha ndege Mzinga mkoani Morogoro kwaajili ya kuwapakia hawa Wabunge wote kuelekea Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupatiwa huduma nyingine zaidi kutokana na majeruhi waliyoyapata", amesema Kamanda Matei.

Pamoja na hayo, Kamanda Matei ameendelea kwa kusema "kati ya hao sita, mmoja amepata majeruhi ya kichwa. Hawa wote ni Wabunge wa Jamhuri Muungano wa Tanzania kutoka Visiwani Zanzibar", amesema Kamanda Matei.

"Chanzo cha ajali hii kimetokana na mnyama aina ya mbwa akiwa anatoka upande mmoja wa barabara na kuelekea upande mwingine na kupelekea dereva aliyekuwa anaendesha gari hilo kushika 'break ya faster' na kusababisha gari hiyo kugeuka ilipokuwa inatokea"amesema kamanda Matei.

Kwa upande mwingine, Kamanda Matei amesema wao kama Jeshi la Polisi hawana tabia ya kuuliza mtu anatokea chama gani wakati wa kutoa msaada kwa kuwa wanaogopa kuonekana wabaguzi katika utoaji wa huduma zao.

No comments:

Post a Comment

Popular