Serikali kugharamia mazishi ya kijana aliyefariki baada ya kutoka polisi. - KULUNZI FIKRA

Tuesday, 27 March 2018

Serikali kugharamia mazishi ya kijana aliyefariki baada ya kutoka polisi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Mbeya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, William Ntinika amefunguka na kuweka wazi kuwa serikali itagharamia mazishi ya kijana Alen Achiles (20), aliyefariki muda mfupi baada ya kutoka polisi.

Mkuu wa wilaya huyo ambaye alifika nyumbani kwa wazazi wa marehemu na kutoa rambirambi ya laki mbili na kuahidi kuwa serikali itagharamia mazishi ya kijana huyo ikiwa pamoja na kukodi gari la matangazo pamoja na chakula.

Hata hivyo Jeshi la polisi mkoani Mbeya limekana kuhusika na kifo cha kijana huyo na kusema kuwa kijana huyo alitoka mikononi mwa Jeshi hilo na kuondoka na ndugu zake baada ya kudhaminiwa akiwa salama.

Mbali na hilo kwa mujibu wa ripoti kutoka hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Mbeya iliyotolewa na Mkurugenzi wa Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Mbeya, Dkt  Godlove Mbwanji, amesema kijana huyo alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo na kueleza kuwa taarifa zilizoandikwa kwenye kitabu cha taarifa za wagonjwa cha hospitali hiyo, zilionyesha kuwa alikuwa amepigwa na kuumia ndani kwa ndani.

Kwa upande wake mama mlezi wa marehemu Alen, Alice Mapunda, ameeleza kuwa wakati wanamchukua kijana wao hospitalini alikuwa analalamika kuwa anajisikia maumivu makali sehemu za tumbo huku akiwa na majeraha mikononi na kichwani, huku mama mdogo wa marehemu, Justina Kilasa, akidai kuwa kijana huyo hakuwa mzurulaji kama inavyodaiwa na Jeshi la polisi na badala yake alikuwa anafanya biashara zake za machungwa na jioni kwenda kanisani.

No comments:

Post a Comment

Popular