Mzungu atetea mfumo wa utawala wa Rais Magufuli. - KULUNZI FIKRA

Sunday, 25 March 2018

Mzungu atetea mfumo wa utawala wa Rais Magufuli.

Mtaalamu  wa masuala ya afya kutoka Ubelgiji anayefanya kazi na moja ya taasisi isiyo ya kiserikali katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dkt Herman Louise Verhofstadt amewakosoa watu hasa kutokea mataifa ya Magharibi wanaokashifu juhudi za Rais John Magufuli katika kuendeleza Tanzania.

Dkt Verhofstadt katika makala yake ya maneno 1,500 aliyoiandika kwenye Mtandao wa Pan African News Hub na kisha kuandikwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii nchini, ameonesha kukerwa zaidi na wachambuzi wa nje wakiwamo wanahabari wanavyomzungumzia Rais Magufuli.

Pia Mzungu huyo alisema kwa muda wa nusu muongo aliokaa nchini, anamuona Rais Magufuli kuwa ni mkombozi wa Watanzania na kiongozi ambaye atalipeleka taifa hili katika uchumi wa kati na wa juu zaidi.

Mtaalamu huyo alianza makala yake kwa kukosoa habari iliyoandikwa katika jarida la Economist ikimkosoa Rais Magufuli na kumfananisha na Rais Donald Trump, kuwa anatimua watumishi kupitia mikutano yake inayorushwa moja kwa moja kwenye televisheni.

Alilikosoa jarida hilo si tu kwa hoja, bali hata marejeo iliyofanya kuhusu kutimuliwa kwa watumishi hao.

Vilevile Mzungu huyo alisema ameshuhudia mabadiliko makubwa ya sera yaliyochochea ukuaji wa uchumi, uimarishwaji wa utawala bora, huduma bora kutokea taasisi za umma na mengineo, katika utawala wa Rais Magufuli.

Aliongeza kuwa Rais Magufuli ameingia madarakani wakati nchi ikiwa imegubikwa na matatizo ya rushwa huku vyombo vya habari vikinunuliwa kusaidia kundi maalumu la watu.

Aliongeza, “Magufuli anawahangaikia wananchi wake kuishi maisha bora kitu ambacho baadhi ya wachumi hawakipendi na kutafutia sababu ya kufanya aonekane ni kama mtu mbaya anayegandamiza demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari na mengine mabaya.”

Aidha, Mzungu huyo alisema katika utawala wa Rais Magufuli ameshuhudia viongozi wakifunguliwa mashtaka mahakamani huku wengine wakifukuzwa kwa kuhujumu mali za umma na taasisi za umma zikiimarika, lakini wachumi wameona kuwa hiyo ni sawa na kazi bure.

Pia alizungumzia harakati za Rais Magufuli za kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia hasa akitolea hatua ya hivi karibuni ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Ulinzi wa Israel, kuwa ni harakati za kuinadi nchi kimataifa zaidi.

Aidha, aligusia sera za Rais Magufuli katika kulinda maliasili na nishati za nchi, ambapo kupitia hilo kwa sasa nchi imeanza kunufaika na madini yake huku kampuni kama Acacia iliyokuwa ikinufaika na madini hayo ikibanwa, Dkt Verhofstadt ameshangazwa na kwa nini wachumi wamekerwa na hatua hiyo.

Mzungu huyo alivitaka vyombo vya habari vya nje kutoandika habari za Tanzania kwa mazoea, akitolea mfano wa kitendo cha vyombo hivyo kukosoa hatua ya serikali ya kuwazuia wasichana wanaopatiwa mimba kuendelea na masomo, akisema kwa mujibu wa tamaduni za Tanzania, hiyo ni sawa.

No comments:

Post a Comment

Popular