Mwigulu Nchemba awaponza wanafunzi Sita UDSM. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 28 March 2018

Mwigulu Nchemba awaponza wanafunzi Sita UDSM.

Wanafunzi sita wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wamelimwa barua za onyo kwa kuhamasisha maandamano kinyume cha sheria.

Wanafunzi hao wanadaiwa kuhamasisha maandamano kutaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ajiuzulu kutokana na kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Aquilina Akwilini, aliyeuawa kwa risasi Februari mwaka huu.

Katika barua yake ambayo imesainiwa na Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma), Profesa David Mfinanga, kwenda kwa wanafunzi hao ambao wamekataa majina yao yasitajwe, imesema onyo hilo ni la mwisho na endapo wataendelea kujihusisha na vitendo hivyo watasimamishwa masomo mara moja kulingana na kipengele 14(xi) wakati mashtaka dhidi yake yakiandaliwa na kushughulikiwa.

“Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, umepata taarifa kuwa wewe ni miongoni mwa wanafunzi wanaojihusisha na vitendo kinyume cha sheria ndogo ndogo za wanafunzi wa Chuo Kikuu ya mwaka 2011, hususan makosa yaliyoainishwa kwenye vipengele 4.2(vxiii), 4.2(xix) na 4.2(xxvi).

“Vitendo hivyo visivyokubalika ni pamoja na kupanga na kuhamasisha maandamano kinyume cha sheria, kujihusisha na vitendo vinavyokishushia hadhi chuo kwa kuanzisha kikundi/vikundi visivyoruhusiwa dhidi ya wanafunzi wenzako, serikali na viongozi wa nchi.

“Kwa barua hii unatakiwa kuacha mara moja vitendo hivi na endapo utakaidi utakuwa umejiongezea makosa mengine kama yalivyoainishwa kwenye sheria ndogo ndogo za wanafunzi wa chuo vipengele vilivyotajwa,” imesema sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo pia imetumwa nakala kwa Makamu Mkuu wa Chuo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma), Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Utafiti), Mwanasheria Mkuu wa Chuo na Kaimu wa Baraza na Mkurugenzi wa Shahada za Awali kwa kumbukumbu.

Akizungumzia barua hiyo, mmoja wa wanafunzi waliopewa barua hiyo amesema barua hizo wamechukua polisi Kituo cha Chuo Kikuu, baada ya kupigiwa simu Machi 14, wakitakiwa kuchukua barua hizo lakini hawakuweza kwa sababu walikuwa wamefunga chuo.

“Kwanza hatukujua wameandika nini, tulipigiwa simu na polisi wa kituo kicho kwamba tukachukue barua zetu tulipoenda tukapewa hizo,” amesema mwanafunzi huyo.

Aidha, amesema barua hizo zimekosewa kwa sababu wao hawakuhamasisha maandamano lakini pia sheria hizo ndogo ndogo zinatoa adhabu kama hiyo kwa mwanafunzi aliyetenda kosa ndani ya chuo.

“Wamekosea hawajataja tulihamasisha maandamano hayo wapi, sisi hatujawahi kufanya maandamano ndani ya chuo sheria hizo zinasema endapo mwanafunzi atatenda kosa ndani ya chuo, hazizui kufanya mwanafunzi kufanya maandamano kitendo cha kusema sisi tulifanya maandamano si kweli.

“Sisi tulifanya mkutano na waandishi wa habari tukasema Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ajipime. Kwa kifupi tumeshachukua hadi kufikia Machi 20, wote tulikuwa tumeshachukua barua zetu na tumejipanga kuzijibu,” amesema.

Hata hivyo, mwanafunzi huyo amesema kuna uwezekani Mwenyekiti wa Mtandai wa Wanafunzi (TSNP), Abdul Nondo naye yake ilikuwapo isipokuwa imeondolewa baada ya kusimamishwa masomo kutokana na kesi ya kutoa taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii na kudanganya kutekwa inayomkabili.



No comments:

Post a Comment

Popular