Mkuu wa mkoa amsimamisha kazi Mganga Mfawidhi. - KULUNZI FIKRA

Tuesday, 20 March 2018

Mkuu wa mkoa amsimamisha kazi Mganga Mfawidhi.

 
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amemsimamisha kazi kaimu mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Kitete, Dkt Nassoro Kaponta kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazoikabili hospitali hiyo zilizotolewa na wananchi.

Uamuzi huo wa Mwanri ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, aliutoa jana baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati hiyo na wafanyakazi wa Hospitali ya Kitete.

Mwanri alisema Dkt Kaponta amesimamishwa si kwa kuwa ametenda kosa, bali ni uwajibikaji wa kawaida kupisha kamati maalumu kufanya uchunguzi wa tuhuma zilizotolewa na wananchi kuhusu mwenendo wa watumishi wa hospitali hiyo ambayo alikuwa akiisimamia.

Alizitaja baadhi ya tuhuma hizo kuwa ni lugha chafu kutoka kwa baadhi ya wauguzi wanazotoa kwa wajawazito, wagonjwa kudaiwa rushwa na baadhi ya wafanyakazi na vifo vya wajawazito vinavyotokana na uzembe.

“Nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu hospitali yetu ya mkoa… tumeamua kumweka pembeni mganga mfawidhi kupisha uchunguzi,” alisema Mwanri.

Alisema wakati uchunguzi ukiendelea, Dkt Kevin Nyakimori atakaimu nafasi ya kaimu mganga mfawidhi hadi uchunguzi utakapokamilika.

Naye mganga mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt Gunini Kamba alisema baadhi ya malalamiko yaliyofikishwa kwake ni kifo cha mfanyakazi wa Hazina ndogo Tabora kilichotokana na kufanyiwa upasuaji na utumbo kujikunja na mwanamke aliyekuwa na upungufu wa damu.

No comments:

Post a Comment

Popular