Meya wa Jiji la Dar es salaam afafanua Juu ya kusifiwa na Makonda. - KULUNZI FIKRA

Sunday, 18 March 2018

Meya wa Jiji la Dar es salaam afafanua Juu ya kusifiwa na Makonda.

Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amesema ameamua kujitoa kafara kukubaliana na tuhuma za usaliti unaotokana na madai ya ukaribu kati yake na viongozi wa Serikali.

Meya Mwita ambaye ni mwanachama wa Chadema alisema nafasi yake ya umeya inamfanya kuwa mbali na majibizano kati yake na Serikali ili kuepuka ukwamishaji wa mipango mbalimbali anayotaka ifanikiwe katika uongozi wake.

“Kwa mfano, kwa sasa tunataka kuleta mabasi ya mwendokasi 110, ukishamaliza kuyaleta, atakayekusainia ni mkuu wa mkoa, akimaliza hiyo taarifa ni lazima ifike kwa Waziri Mkuu ili aweze kuipitisha, ”alisema meya  Mwita Jana alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu tuhuma za usaliti.

Jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alimmwagia sifa meya huyo huku uongozi wa Chadema ukipongeza busara inayoonyeshwa na Mwita katika kufanya kazi na uongozi wa mkoa huo.

Katika Mkutano wa kuzindua Mpango wa Kuendeleza Utalii Makonda alisema meya  Mwita ni kiongozi anayefanya kazi, mwenye dhamira ya kutumikia wakazi wa jiji hilo na mfano kwa mameya wa upinzani wanaotaka kufanya kazi naye badala ya kuendelea kutukana matusi kwa mkuu wa nchi.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt Vicent Mashinji alisema meya Mwita ameendelea kuonyesha taswira ya viongozi katika kufanya kazi na viongozi wa Serikali ya mkoa huo.

No comments:

Post a Comment

Popular