Katibu mkuu wa Chadema afunguka kuhusu Jeshi la polisi. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 22 March 2018

Katibu mkuu wa Chadema afunguka kuhusu Jeshi la polisi.

 
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Katibu Mkuu wake Dkt Vicent Mashinji amesema wanafanyiwa usumbufu na Jeshi la Polisi wa kuitwa kila wiki na mwishowe hakuna jambo jipya wanaloambiwa wanapokuwa wameitikia wito wa kuripoti.

Dkt Vicent Mashinji ametoa kauli hiyo muda mchache alipotoka nje ya kituo cha Polisi 'Central' Jijini Dar es Salaam Leo (Machi 22, 2018) baada ya kuitikia wito wa Kipolisi kama walivyotakiwa kufanya hivyo awali kwa lengo la kuhojiwa juu ya tuhuma za kufanya mkusanyiko usiokuwa halali.

"Jambo moja nataka niwakumbushe watanzania wenzangu kwamba Tanzania tunakitu kinachoitwa kiingereza 'Police Force' hatuna 'Police services' yaani maana yake tuna Jeshi la Polisi la kusukuma watu nasio la kutoa huduma mbalimbali kwa jamii", amesema Dkt Mashinji.

Pamoja na hayo, Dkt Mashinji ameendelea kwa kusema "kila bada ya siku tatu nne tunakuja, tunakaa hapa hakuna jambo lolote la maana linalofanyika kwa hiyo inaonekana tu kwamba ni usumbufu tu".

"Muda mwingine mtu anapoamua kukusumbua tu unampa fursa tu naye ajisikie tu raha afanye kile anachojisikia, kimsingi hakuna jambo lolote tunalolivunja kisheria zaidi ya wao ya usumbufu mara kwa mara. Sisi tutaendelea kuripoti kulingana na wao wanavyotaka" amesema Dkt Mashinji.

Kwa upande mwingine, viongozi wa Chadema wametakiwa kurudi tena kituo cha Polisi Jijini Dar es Salaam siku ya Jumanne Machi 27 mwaka 2018.

No comments:

Post a Comment

Popular