Wanafunzi zaidi ya 300 wameweka kambi nje ya ofisi za Bodi ya mikopo baada ya kunyiwa mikopo - KULUNZI FIKRA

Tuesday, 7 November 2017

Wanafunzi zaidi ya 300 wameweka kambi nje ya ofisi za Bodi ya mikopo baada ya kunyiwa mikopo

 
 Zaidi ya wanafunzi 300 wa vyuo mbalimbali wameweka kambi nje ya ofisi za bodi ya mikopo baada kukosa mkopo huku wakiwa na vigezo.

Baadhi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu wamekwenda ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kushinikiza wapewe mikopo ili wafanye usajili kwa mwaka wa masomo 2017/18.

Wanafunzi hao wamekusanyika toka juzi Jumatatu Novemba 6,2017 katika ofisi za HESLB zilizoko Mwenge jijini Dar es Salaam, hivyo kusababisha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kufika eneo hilo.

Baadhi ya wanafunzi waliangua vilio walipozungumzia tabu wanazopata kutokana na majina yao kutoonekana katika orodha ya wanaopata mikopo.

Mwanafunzi, Nillan Liunga amesema hajui hatima yake kwa kuwa fedha alizonazo zinakaribia kwisha na hana ndugu jijini Dar es Salaam.

"Maisha yenyewe naishi ya kuungaunga nimetoka Mbeya nimefikia gesti. Sina wazazi, nimesoma kwa shida licha ya kuwa na vigezo vyote vya kupewa mkopo mpaka sasa sijui nini hatima yangu," amesema Liunga.

Wanafunzi hao wametakiwa na maofisa wa HESLB kuorodhesha majina yao jambo ambalo wamesema halijawaridhisha.

"Kama tulituma maombi mtandaoni hawajatupa mkopo, hayo majina ya kwenye karatasi watayatumia kweli? au ndiyo wanatudanganya," amehoji mwanafunzi Christopher Mwita.

Mwita amesema kwa chuo alichochaguliwa anatakiwa kulipa asilimia 50 ya ada ili asajiliwe na muda wa usajili unakwisha ndiyo maana amefika ofisi za HESLB kujua hatima yake.

"Ijumaa ndiyo usajili unafungwa lakini sisi tumeambiwa tusubiri Jumatatu ndipo watatangaza utaratibu wa kukata rufaa," amesema Mwita.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa HESLB, Omega Ngole amesema jukumu lao ni kuwapokea na kusikiliza hoja za wanafunzi hao kabla ya kuzifanyia kazi.

Amesema wamewataka wanafunzi hao kuorodhesha majina ili waangalie ni wapi walikosea na kuwapa majibu au kufanyia kazi changamoto zao.

“Tunaendelea kuifanyia kazi orodha ya majina tuliyopokea kutoka Tume ya Vyuo Vikuu (TCU). Majina wanayoandika leo pia tutayafanyia kazi, hadi Ijumaa tutatoa orodha ya nne ya wanufaika wa mikopo wenye sifa,” amesema Ngole.

Amesema wanafunzi wanaolalamika ikibainika kuna wenye sifa za kupata mkopo kutokana na vigezo vilivyotajwa, wameomba kwa usahihi na wameambatanisha kila kinachohitajika, watasaidiwa kwa kila hali.

“Wiki ijayo tutafungua rasmi dirisha la kukata rufaa, hivyo wanafunzi wenye malalamiko yakiwemo ya kupata mikopo midogo na kunyimwa ilihali wanastahili watapata fursa ya kusikilizwa,” amesema Ngole.

No comments:

Post a Comment

Popular