Wabunge wa CCM wamkingia kifua Rais Magufuli Bungeni. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 9 November 2017

Wabunge wa CCM wamkingia kifua Rais Magufuli Bungeni.

 WABUNGE wa CCM wamemkingia kifua Rais John Magufuli bungeni kuwa hajipendelei anapofanya ziara kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa, bali inatokana na sababu kadhaa ikiwemo kubana matumizi anapokuwa na ziara nje ya nchi, ambako hutumia gari.

Ufafanuzi kuhusu ziara kadhaa zilizofanywa na Rais Magufuli Kanda ya Ziwa umetokana na wabunge wa Chadema, Peter Msigwa wa Iringa Mjini aliyedai Rais anapendelea mikoa ya Kanda ya Ziwa na amekuwa akifanya ziara sana huko pamoja na kupeleka fedha bila kufuata taratibu za ujenzi wa uwanja wa ndege wa Chato.

Pia Joseph Mbilinyi wa Mbeya Mjini alidai Rais Magufuli hakuwahi kufanya ziara mkoani Mbeya na hata hivi karibuni kwenye mkutano wa Jumuiya ya Serikali ya Mitaa (ALAT) uliofanyika mkoani humo, Rais hakwenda na alituma mwakilishi hivyo kumtaka aende mkoani humo.

Kutokana na kauli hizo, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kisheku ‘Musukuma’(CCM) akaomba mwongozo na kueleza kuwa, “Kauli za Msigwa na Sugu juu ya ziara ya Rais Magufuli Kanda ya Ziwa inatukarahisha sisi watu wa kanda hiyo kwani Rais hastahili kutembelea kwetu?”

“Rais amekuja kwetu akiwa njiani anapita anakwenda Uganda na anatumia gari hivyo anaokoa fedha, lakini pia anakuja Kanda ya Ziwa mapumzikoni kwani ni kwao na ana ndugu na jamaa anatakiwa kuwatembelea na sijaona rais yeyote anapokuwa mapumzikoni anakwenda mkoa mwingine, Msigwa asubiri rais atakapokwenda Iringa.”

Aliwataka wabunge hao kuacha ukanda na kusisitiza, “sisi mbona hatusemi wao (Chadema) wanapeana ubunge kwa ushemeji na kuwaleta humu wachumba zao”. Naye Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan ‘Zungu’ akawataka wabunge kuwa na tahadhari na kujipima kwa maneno yao wanayoyatoa bungeni.

“Rais (Magufuli) ana ziara Uganda na anatumia gari hivyo amepita tu huko kama njia na ni katika sehemu ya kubana matumizi,”alisema. Wakati huo huo, Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM) amesema mitandao ya kijamii ya Instagram na WhatsApp imekuwa ikitumika nchini kutangaza biashara ya ngono, mapenzi ya jinsi moja, inatumika kutoa taarifa za uongo na kutolea mfano wa Mbunge(hakumtaja) aliyetuma barua ya kujiuzulu inayokwenda kwa Spika kupitia Instagram.

Aliomba mwongozo kuelezwa kazi ya kudhibiti ni ya Wizara ya Habari au Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kwani maadili yamekuwa yakiporomoka kwa kasi. Hata hivyo, Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama alijibu kuwa:

“tumemsikia mbunge, serikali itaendelea kutoa ufafanuzi wa kisheria na kutoa elimu katika kuboresha maadili”. Akichangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti ya serikali kwa mwaka 2018/2019 uliowasilishwa juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, Mbunge wa Mbulu Vijijini, Zakaria Isaya(CCM) alimtaka Rais Magufuli kutolegeza uzi kwenye uongozi wake kwani nchi haitaki mzaha.

Alitaka baadhi ya watendaji serikalini kuondolewa ambao hawasajibiki ipasavyo na watoa kauli mbaya kwa wananchi wanaokwenda kwenye ofisi za serikali. “Mtendaji anachukua mwezi mmoja kutoa faili kwenye meza moja kwenda nyingine, hawajibiki, anatoa kauli chafu kwa mwananchi, haendani na kasi ya serikali ya awamu ya tano, hao waondolewe mara moja,”alisema.

Alishauri ukusanyaji mapato uboreshwe ili umfanye mlipakodi mzalendo na rafiki kwa serikali tofauti na sasa unamkandamiza mlipakodi. Mbunge wa Nachingwea, Hassan Masala (CCM) ameilaumu Wizara ya Kilimo ya kufanya utafiti na kutafuta masoko kwa kushindwa kutafuta masoko ya mbaazi ya wakulima na kukaa kimya wakati wakulima walishahamasishwa kuzalisha kwa wingi zao hilo.

“Waziri wa Kilimo atoe tamko juu ya kukosa soko la mbaazi, sasa hivi kilo moja inauzwa Sh 150 sasa tuambiwe msimu ujao zitahitajika mbaazi tani ngapi ili tusiwalazimishe wakulima kulima kwa wingi wakakosa tena soko na kama india imevunja mkataba wa kununua mbaazi mseme,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Popular