Ujenzi wa ukuta Mererani wapamba moto, Waziri Mwinyi autaka ndani ya muda wa miezi sita. - KULUNZI FIKRA

Saturday 4 November 2017

Ujenzi wa ukuta Mererani wapamba moto, Waziri Mwinyi autaka ndani ya muda wa miezi sita.

 Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi amelitaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linalojenga ukuta unaozunguka mgodi wa madini ya Tanzanite eneo Mererani wilayani Simanjiro kutekeleza chini ya muda wa miezi sita.

Amesema hayo Juzi  katika ziara ya kukagua maandalizi ya ujenzi huo eneo la Mererani ambao unalenga kudhibiti utoroshwaji wa madini Tanzanite yanayopatika nchini Tanzania pekee.

Ujenzi huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais John Magufuli aliyoyatoa mwezi Septemba na kuiagiza JKT kujenga ukuta ndani ya kipindi cha miezi sita.

“Nataka kazi hii ambayo mheshimiwa Rais amewapa itekelezwe katika kipindi kifupi zaidi na iwe na ubora wa kiwango cha juu, hii kazi ya ujenzi wa ukuta itakua ni kipimo chenu kwa ajili ya kupewa kazi nyingine kubwa,” alisema Dk Mwinyi.

Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Michael Isamuhyo alisema maandalizi ya ujenzi huo yamekamilika na wamepata ushirikiano mzuri kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Kijiji cha Naisinyai.

Alisema watatekeleza maelekezo aliyoyatoa na kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kabla ya kipindi walichopewa.

Kamanda wa Operesheni ya ujenzi wa ukuta huo, Kanali Festus Mang’wela alisema Mkuu wa JKT atazindua rasmi ujenzi huo Novemba 6 na utakamilika katika kipindi cha miezi sita.

Alisema fedha zote za ujenzi kiasi cha Sh 4.8 bilioni zimeshatolewa na vikosi 20 vya askari wa JKT vimeshawasili kutekeleza maagizo ya Rais Magufuli.

Awali Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alisema ujenzi wa ukuta huo utasaidia kuokoa kiwango kikubwa cha madini ya Tanzanite yanayopatika nchini pekee kulinufaisha Taifa.

“Kwa kipindi kirefu sekta ya madini ilichukuliwa kama ni huduma badala ya biashara na wakati mwingine baadhi ya watumishi walishirikiana na wezi kuliibia Taifa letu,” alisema Profesa Msanjila.

Alisema ukuta ni sehemu ya ulinzi lakini wizara yake itatoa elimu kwa watumishi wake na Wananchi kuwa na tabia za uzalendo kwa maslahi mapana ya kulinda rasilimali za Taifa.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Naisinyai, Taiko Laizer alisema watashirikiana na JKT kutekeleza mradi huo na wameshaanza kunufaika na ujenzi huo baada ya Zahanati ya kijiji hicho kupokea maofisa afya wa kutosha watakaotoa huduma kwa askari na wananchi.

No comments:

Post a Comment

Popular