Ruvuma: Mkuu wa polisi Tunduru aamuru kukamatwa kwa askari polisi anayewanyanyasa wananchi. - KULUNZI FIKRA

Saturday 4 November 2017

Ruvuma: Mkuu wa polisi Tunduru aamuru kukamatwa kwa askari polisi anayewanyanyasa wananchi.

 
 Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Tunduru mkoani ruvuma, mrakibu mwandamizi wa jeshi la polisi, Bw. Nico Mwakasanga ameamuru kukamatwa kwa askari polisi mmoja aliyejulikana kwa jina la Bw. Mbunda na kuwekwa ndani kwa uchunguzi zaidi mara baada ya baadhi ya wananchi wa wilaya ya tunduru kutoa malalamiko yao kwa mkuu wa mkoa wa ruvuma, Mh.Christina Mndeme kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji na askari huyo.

Wakitoa malalamiko hayo kwa mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Mh. Christina Mndeme ambaye kwa mara ya kwanza amefanya ziara ya kikazi wilayani Tunduru tangu kuteuliwa kwake Octoba 6 mwaka huu kuwa mkuu wa mkoa wa Ruvuma, baadhi ya wananchi hao wa Tunduru wamesema askari huyo amekuwa akiwanyanyasa kwa kuwabambikiza kesi na wakati mwingine kukamata wananchi wakiwa kwenye shughuli za uzalishaji mali akiwaita wazurulaji.

Akijibu malalamiko hayo ya wananchi, mkuu wa Polisi wa wilaya ya Tunduru, Mrakibu Mwandamizi wa jeshi la Polisi,Bw. Nico Mwakasanda amesema ameshaagiza askari Polisi huyo akamatwe popote alipo na kuwekwa ndani kwa uchunguzi zaidi.

Hata hivyo mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Mh, Christina Mndeme amewaonya askari polisi kuacha tabia ya kubambikizia kesi wananchi na badala yake watende haki huku akiwataka wananchi wasiogope kutoa taarifa polisi endapo wanafanyiwa vitendo hivyo ili hatua zaidi zichukuliwe.

No comments:

Post a Comment

Popular