Mwanza: Madiwani na watendaji wa Jiji pamoja na waandishi wa habari wameshambuliwa na wananchi kwa mawe. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 8 November 2017

Mwanza: Madiwani na watendaji wa Jiji pamoja na waandishi wa habari wameshambuliwa na wananchi kwa mawe.

 
Madiwani, Watendaji wa jiji la Mwanza na waandishi wa habari waliokuwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na maeneo yenye migogoro ya ardhi wamelazimika kutimua mbio kujiokoa kutoka mikononi mwa wakazi wa Kata ya Mahina waliokuwa wakiwashambulia kwa mawe.

Pamoja na mawe, wakazi wa Kata hiyo inayowakilishwa na Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire pia walijihami kwa kubeba silaha za jadi yakiwemo mapanga, rungu na fimbo.

Tukio hilo limetokea leo Jumatano Novemba 8,2017 baada ya msafara huo wa watu zaidi ya 30 uliokuwa na magari matatu kufika Mtaa wa Mahina inakojengwa Zahanati ya Meya Bwire katika kiwanja kinachodaiwa kuwa cha umma kilichotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Serikali

Mkuu wa msafara, Dismass Litte ambaye ni diwani wa Mkolani hakuwa tayari kuzungumza tukio hilo kwa maelezo kuwa litajadiliwa na kutolewa ufafanuzi baada ya kikao chao cha ndani kinachoendelea usiku huu katika ukumbi wa jiji.

Waandishi wa habari waliokuwa wakipiga picha tukio hilo nao walilazimika kukimbia baada ya kundi lingine liliojificha kuibuka na kutaka kuwapora kamera.

"Kwa jinsi tukio lilivyotokea, Vijana waliotushambulia wameandaliwa ndiyo maana waliweka mtego kwa kulizunguka eneo la tukio na kuanza kurusha mawe", alisema diwani wa Igogo, John Minja akizungumzia tukio hilo.

Tukio hilo limetokea kukiwa na mgogoro kati ya Meya Bwire na baadhi ya viongozi wa Jiji la Mwanza ambao Rais Magufuli ameagiza umalizwe kwa njia ya majadiliano.

Madiwani 20 wa jiji tayari wamewasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Meya wakimtaka kuachia ngazi.

No comments:

Post a Comment

Popular