Meya wa manispaa ya Kigoma : Nachukulia tishio la Waziri Mkuchika kama vita dhidi ya watu wa manispaa yetu. - KULUNZI FIKRA

Monday, 13 November 2017

Meya wa manispaa ya Kigoma : Nachukulia tishio la Waziri Mkuchika kama vita dhidi ya watu wa manispaa yetu.

Nimeshtushwa, kushangazwa na kuchukizwa na tishio la kuivunja Halmashauri ya Manispaa ambalo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa leo bungeni. Waziri wa Utawala Bora alikuwa anajibu swali la mbunge wetu wa Kigoma Mjini kuhusu uamuzi wa Serikali kujitoa katika Mpango wa Uendeshaji wa Serikali kwa uwazi ( OGP ). Waziri George Mkuchika ameionya Manispaa yetu kuwa isipojitoa OGP itavunjwa na badala yake kuundwe Tume ya Manispaa.

Nikiwa Meya wa Manispaa hii nachukulia tishio hili la Waziri kwa uzito mkubwa na ni tangazo la vita dhidi ya watu wa Manispaa ya Kigoma Ujiji. Mnamo mwezi Februari mwaka 2016 Manispaa yetu ilishindana na Miji mingine 45 duniani kuchaguliwa kuwa waanzilishi wa program ya Uendeshaji wa Serikali za Mitaa kwa uwazi. Miji 15 ilichaguliwa ikiwamo Manispaa yetu. Shindano hili halikuwa na mahusiano yeyote na uanachama wa Tanzania kwenye OGP. Hivyo Manispaa yetu ilijiunga na OGP kwa kujitegemea na wala hatukuhitaji hata barua ya Serikali Kuu kutuidhinisha.

Serikali kutulazimisha kujitoa kwa sababu tu wenyewe wamejitoa ni kinyume cha demokrasia, kutuingilia mambo yetu na ni njama za kutukwamisha kwa sababu za kisiasa. Manispaa yetu inapata faida kubwa kuwa mwanachama wa OGP SubNational. Watendaji wetu wamejengewa uwezo, idara yetu ya ardhi inawezeshwa vifaa vya kisasa vya kuhifadhi kumbukumbu za wamiliki wa ardhi na kuondoa kabisa migogoro ya ardhi kwenye manispaa, wananchi wanapata taarifa za mapato na matumizi ya manispaa yao kwa kuweka wazi kila fedha inayoingia na taarifa ya robo mwaka ya ukaguzi wa ndani ( www.kigomaujijimc.go.tz ). Vile vile tumeweza kujenga mtandao wa mahusiano na Miji kama Bojonegoro wa Indonesia, Madrid ya Hispania, Paris ya Ufaransa, Ontario ya Canada na Sekondi Tokoradi ya Ghana. Kuwa kwenye OGP SubNational kumewezesha watu wenye mitaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia kutaka kuwekeza kwenye Manispaa yetu.

Mfano kesho Manispaa inaingia makubaliano na kampuni ya LingHang Group ya kuwekeza Kituo cha Biashara cha Maziwa Makuu ( The Ujiji City ) na Kiwanda cha Samaki cha Katonga. Vile vile kampuni ya HITACHI ya Japan inawekeza kuzalisha umeme wa jua kuendesha mitambo ya Maji kwenye manispaa, uwekezaji wa Utalii wa matibabu ( medical tourism) nk.

Kwa hakika kutulazimisha kujitoa OGP ni kupunguza nafasi yetu ya ushawishi duniani. Nikiwa Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, nimefanya juhudi za kuwasiliana na Serikali Kuu ili kupata ufafanuzi na kuitaka Serikali ituache tuendelee kutekeleza Mpango Mkakati wetu wa OGP. Hata hivyo Serikali haikunipa majibu yeyote mpaka leo tuliposikia Bungeni tukionywa kuacha kuwasiliana na watu wa OGP.

Tunashangazwa na hatua hii ya Serikali inayojitanabaisha kwa kupambana na ufisadi. Uwazi ni dawa endelevu dhidi ya ufisadi. Baraza la Madiwani la Manispaa ya Kigoma Ujiji litakaa na kujadili suala hili na kufanya maamuzi yenye kujali maslahi mapana ya Mji wetu.

Hussein Ruhava
Meya Manispaa Kigoma Ujiji
13/11/2017

No comments:

Post a Comment

Popular