Kubenea ataka serikali kuwachukulia hatua viongozi wote waliohusika kuifilisi TTCL. - KULUNZI FIKRA

Tuesday, 14 November 2017

Kubenea ataka serikali kuwachukulia hatua viongozi wote waliohusika kuifilisi TTCL.

MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea, ameitaka serikali kuwakamata na kuwafikisha mahakamani, watumishi wa umma na wanasiasa waliochangia kufilisika kwa shirika la simu la taifa (TTCL).

Akizungumza bungeni mjini Dodoma leo Jumanne, Kubenea alisema, kampuni ya simu ya TTCL ilifilisika kutokana na kuhujumiwa na baadhi ya watu wenye mamlaka serikalini.

Kubenea amesema, kwa mujibu wa rekodi na taarifa zilizopo serikalini, muwekezaji aliyopewa TTCL wakati huo, alishindwa kutimiza masharti ya mkataba, lakini serikali iliendelea kumbeba na kumkumbatia.

Mbunge huyo machachari wa Chadema alikuwa alitoa kauli hiyo wakati aakijadili muswaada wa kuanzisha Shirika la Simu la umma (The Tanzania Telecommunications Bill, 2017).

Katika mchango wake huo, Kubenea alinukuu kauli ya aliyekuwa waziri wa Mawasiliano na uchukuzi, Prof. Mark Mwandosya aliyesema kuwa ubinafsishaji wa mashirka ya umma ilifanyika kutokana na serikali kushindwa kuyaendesha.

Kubenea alisema, Prof. Mwandosya alionya kuwa pamoja na dhamira njema ya kuanzisha mashirika ya umma, lakini kuyaendesha mashirika hayo na kuyasimamia, ni jambo lisilowezekana.

“Serikali iliamua kubinafsisha TTCL baada ya kujiridhisha kuwa teknolojia ilikuwa imebadilika na kuliendesha kunategemea ruzuku kutoka serikalini. Kulirudisha leo, ni kujipeleka mbele na kujirudisha nyuma,” ameeleza Mhe Kubenea.

No comments:

Post a Comment

Popular