Jukwaa la katiba Tanzania kugonga mahakamani kudai haki ya kuandamana. - KULUNZI FIKRA

Sunday 5 November 2017

Jukwaa la katiba Tanzania kugonga mahakamani kudai haki ya kuandamana.

 Jukwaa la Katiba nchini Tanzania (JUKATA) limesema litafungua kesi mahakamani kupinga kuzuiwa maandamano ya amani yaliyolenga kushinikiza kuendelea kwa mchakato wa Katiba Mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumamosi, Novemba 4,2017, Mwenyekiti wa JUKATA, Hebron Mwakagenda amesema wamefikia uamuzi huo baada ya sababu zilizotolewa na polisi kuzuia maandamano hayo kuwa nyepesi.

“Tumefikia uamuzi wa kwenda kufungua kesi mahakamani kudai haki ambayo inaminywa na kukandamizwa na Jeshi la Polisi kwa kutumia sababu nyepesi..Tupo katika hatua za mwisho kutekeleza uamuzi huu na jopo la mawakili wasomi wasiopungua 10 watahusika kudai haki ya kufanya maandamano ya amani,” amesema Mwakagenda.

Hata hivyo, Mwakagenda amesema polisi katika barua ya kuzuia maandamano imeeleza kuwa, Rais John Magufuli ambaye JUKATA ilimuomba kupokea maandamano hayo hajatoa tamko lolote kuhusu maandamano hayo. Huku jeshi la polisi likikataa maandamano hayo kwa sababu tatu umbali wa maandamano hayo ambapo JUKWATA walipanga kuandamana kuanzia Mwenge hadi Mnazi Mmoja, na kudai kuwa siku hiyo ya tarehe 30 Oktoba ilikuwa ni siku ya mitihani ya kidato cha nne.

Mapema mwezi Oktoba mwaka huu Jukwaa hilo lilitangaza kufanya maandamano ya amani nchi nzima tarehe 30 Oktoba ,2017 kushinikiza kuanza kwa mchakato wa kudai katiba mpya.

No comments:

Post a Comment

Popular