Mbunge Peter Msigwa alilia ongezeko mshahara kwa madiwani - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 4 October 2017

Mbunge Peter Msigwa alilia ongezeko mshahara kwa madiwani

 Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, mchungaji Peter Msigwa, amesema upo umuhimu wa kuongeza mshahara kwa madiwani waliopo nchini kutokana na kazi kubwa wanayoifanya viongozi hao.

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio Jana  Jumatano Oktoba 4, kiongozi huyo ametolea mfano kwenye Halmashauri ya Iringa Mjini, kwa kusema madiwani wa eneo hilo hulipwa shilingi 40,000 kwa kila kikao kimoja na nauli shilingi 10,000.

“Madiwani wanafanya kazi kubwa sana na ukiangalia kiinua mgongo chao baada ya miaka mitano, hakizidi milioni 12,”

Msigwa amebainisha mshahara anaolipwa diwani kwa kila mwezi kuwa ni shilingi 350,000 na kuongeza kuwa kuna utofauti wa malipo ya posho kwa viongozi hao wa kata, kutokana na makusanyo yanayopatikana kwenye halmashauri husika.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano mkuu wa 33, wa Jumuia ya Tawala za mitaa Tanzania (ALAT), jana Jumanne, rais John Magufuli, amesema hatoongeza mishahara, huku akiwataka madiwani wasiokuwa na vyanzo vya kipato, wajiuzulu.

“Na ndiyo maana mimi mishahara waliokuwa wanapata wengine sikupandisha na sitapandisha, kwa sababu ninawajibu wa kuwatumikia watanzania kwanza, na kazi ya udiwani masharti tunapojaza fomu, tunaambiwa lazima uwe na kazi maalum inayokupa kipato,” alisema kiongozi huyo.

“Sasa kama wapo madiwani waliojaza hiyo nafasi na hawana kazi ya kuwapa kipato, ni afadhali wajiuzulu udiwani” aliongeza Dkt. Magufuli.

No comments:

Post a Comment

Popular