Askari wa JWTZ agonga basi la mwendokasi na kusababisha madhara makubwa kwa abiria - KULUNZI FIKRA

Friday, 27 October 2017

Askari wa JWTZ agonga basi la mwendokasi na kusababisha madhara makubwa kwa abiria

 
 Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amegonga basi la mwendokasi na kusababisha madhara kwa abiria na basi, huku akikimbia na kutelekeza gari alilokuwa akiliendesha.

Tukio hilo limetokea juzi maeneo ya Magomeni jijini Dar es salaam, baada ya dereva wa gari hilo kuingia kwenye barabara ya mwendokasi kisha kugongana na basi lililokuwa na abiria.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo huku akiwataka madereva wote bila kujali ni taasisi gani kufuata sheria za nchi na kuacha kutumia mabavu.

Mambosasa alisema dereva huyo alifanya makosa kwa kuingia njia ya mabasi yaendayo kasi huku akijua kuwa kufanya hivyo ni kosa kinyume cha sheria.

"Huyu dereva ana makosa, kwanza alishindwa kuheshimu taa zinazoongoza magari na hairuhusiwi kupita katika njia hizo za mwendokasi. Baada ya kusababisha ajali hiyo, alilitelekeza gari na kukimbia", alisema Mambosasa.

"Namba za gari la jeshi (JWTZ) kwa sasa sizikumbuki kwa kuwa nimetoka ofisini nashughulika na masuala ya mafuriko".

Kuhusu madhara ya ajali hiyo, alisema watu wachache waliumia na kupelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu na baadaye kuruhusiwa.

Mambosasa alisisitiza kuwa madereva wa majeshi wanatakiwa kufuata sheria za nchi bila kutumia mabavu ama cheo.

"Nilishasema hakuna ambaye yuko juu ya sheria. Ni vizuri hao madereva wa Jeshi wakafuata sheria za barabarani na hairuhusiwi kutanua kwenye barabara ambayo si njia yako", alisema Kamanda Mambosasa.

Aidha, alisema kuna magari ambayo ni dharura yaliyoruhusiwa kupita kwenye njia ambayo si yake kinyume cha hapo, mengine yote yanatakiwa kufuata sheria zilizopo.

Kulunzifikra blog ilishuhudia gari ya Jeshi ikipita katika njia ambayo si yake katika eneo la Riverside Ubungo na kumgonga mwendesha bodaboda ambaye alikuwa kwenye njia yake.

No comments:

Post a Comment

Popular