Simba ya Omog yashtua wakubwa - KULUNZI FIKRA

Saturday, 23 September 2017

Simba ya Omog yashtua wakubwa

 NAMBA hazidanganyi. Mwenendo wa Simba msimu huu huenda usiwe mzuri kwani rekodi zinaonyesha haijawahi kupata pointi chache kama sasa kwenye mechi nne za awali za msimu tangu mwaka 2014.

Simba iliuanza msimu huu kwa kasi iliposhinda 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, lakini baada ya mechi nne kukamilika, imekusanya alama nane tu, chache zaidi kukusanywa na timu hiyo katika miaka mitatu iliyopita.

Simba imeshinda michezo miwili na sare mbili, ikiwa ni wastani usioridhisha tangu 2014 ilipopata sare nne mfululizo na kukusanya alama nne tu. Wakati huo ilikuwa chini ya kocha Patrick Phiri raia wa Zambia.

Mwaka 2015 ilikusanya alama tisa baada ya mechi nne za awali iliposhinda dhidi ya African Sports, JKT Mgambo na Kagera Sugar kisha kupoteza mchezo mmoja tu dhidi ya Yanga wakati huo kocha akiwa Mwingereza, Dylan Kerr.

Mwaka jana ikiwa chini ya Omog ilikusanya alama 10 katika mechi nne za mwanzo iliposhinda mara tatu na kutoa sare moja dhidi ya JKT Ruvu. Ilipata matumaini.

Rekodi zinaonyesha katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Simba ilianza vizuri msimu wa 2012/13 ilipopata alama 12 katika mechi nne za mwanzoni, ilishinda dhidi ya African Lyon, Ruvu Shooting, JKT Ruvu na Prisons.

Maswali yanabaki juu ya uwezekano wa Simba kuendeleza wimbi la ushindi sasa.

Yanga nayo

Rekodi zinaonyesha msimu huu umekuwa mbovu kwa Yanga tangu mwaka 2013. Imeshinda mchezo mmoja na kutoa sare mbili katika mechi tatu za awali, hivyo kupata alama tano, sawa na ilizopata mwanzoni mwa msimu wa 2013/14 ilipoishinda Ashanti United na sare za Coastal Union na Mbeya City.

Kiwango bora zaidi kwa Yanga katika mechi za mwanzoni katika miaka mitano iliyopita ni mwaka 2015 ambapo ilikusanya alama tisa baada ya kushinda mechi zote tatu za mwanzoni dhidi ya Coastal Union, Prisons na JKT Ruvu.

No comments:

Post a Comment

Popular