Serikali inavyojipalia makaa - KULUNZI FIKRA

Saturday, 30 September 2017

Serikali inavyojipalia makaa

 TUNA Serikali iliyopendwa na watu tangu ilipoingia madarakani. Ni Serikali  iliyoungwa mkono kwa kiasi kikubwa kutokana na kufufua matumaini ya Watanzania ya kupata maisha bora.

Kukubalika kwake kulifanya hata watu  waamini hakuna haja ya kuwa na upinzani!

Kuna wakati watu walikuwa wakijiuliza, ikiwa Serikali inachukua hatua kupambana na ufisadi, wapinzani watabeba ajenda gani tena? Ajabu ni kwamba Serikali hiyo hiyo imekuwa ikichukua hatua za kushusha umaarufu wake na kusaidia kuujenga upya upinzani ambao ulikuwa unadhoofika.

Serikali imewapatia wapinzani ajenda mpya ya kusimamia – ajenda kuminywa kwa ya uhuru na haki za kisiasa na kiraia! Hii ni kwa sababu Serikali imekuwa ikichukua hatua ambazo zinaonekana zina mushkeli kwake kisiasa, ikiwemo marufuku za mikutano, kamatakamata ya wapinzani, kibano bungeni nk.

Kila nikiangalia, naona uungwaji mkono wa Serikali unazidi kushuka na upinzani unapata nguvu. Naamini, Serikali ya awamu ya tano ingeacha wapinzani wafanye kazi zao kwa uhuru huenda upinzani usingekuwa na nguvu, kama hivi sasa.

Natamani serikali ingeelewa kuwa kila baya linalofanywa dhidi ya wapinzani ni simenti inayouimarisha na kuvutia huruma zaidi za watu. Nakaa, najiuliza, kwa nini?

Wapinzani  nao!

Wapinzani nao! Wana mengi ya kushangaza lakini kubwa ni kukosa mbinu za kisiasa na kuishia kupinga kila kitu. Wakati Rais John Pombe Magufuli anatangaza vita ya uchumi, na akiingia katika mapambano na wawekezaji wanyonyaji, wapinzani walitabiri kushtakiwa na kuita upuuzi taarifa za wasomi wetu waliobobea waliofanya uchunguzi.

Labda kweli taarifa zina mapungufu, lakini ni sahihi kuziita upuuzi, wakati watu walijipinda kuziandaa kiuzalendo kabisa? Na kwa kuita upuuzi, hata ukawa ni upuuzi kweli, unamsaidia nani? Watanzania au wawekezaji wa nje?

Uzalendo hupimwa zaidi kwa mashikamano wa taifa dhidi ya adui wa nje. Hata kama kuna kosa upande wenu, unasimama kutetea upande wako! Somo hilo ni gumu kwa wapinzani.

Na ukweli ni kwamba hata ingekuwa imetiwa chumvi, taarifa za makinikia zilisaidia kulazimisha wawekezaji waje mezani kwa sababu inachafua taswira yao duniani na kuimarisha dhana kuwa makampuni hayo ni mirija ya nchi tajiri ya kunyonya rasilimali zetu bure.

Pia, ukiwa katika meza ya majadiliano, kama unataka ulipwe mia lazima uanze kwa kudai alfu. Baadhi ya hoja za wapinzani zilionesha hata kujidharau, kama vile tunasema: “Mzungu hawezi kuiba, ingekuwa Muafrika sawa.”

Spika na madaraka yasiyoandikwa

Unajua kwa nini nchi zina katiba, sera, sheria na kanuni za kundesha mambo? Ni kwa sababu ya kudhibiti matumizi mabaya ya ofisi. Njia moja ambayo ofisi inaweza kutumika vibaya ni pale viongozi wanapotumia madaraka yao kulipa visasi binafsi, kinyume na utaraibu.

Lakini tumepata somo tofauti kidogo hapa Tanzania, pale Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania, Job Ndugai, aliposema ana uwezo wa kumzuia mbunge kuzungumza kipindi chote cha ubunge wake, hata kama hilo halijatajwa popote katika sheria na kanuni.

Ndugai alinukuliwa akisema: “Kiongozi wako wa kazi ana mamlaka makubwa kuliko yaliyoandikwa, na madaraka pia.  Sio kila jambo lazima iwe ni kanuni. Narudia tena. Nimesikia watu wakibishabisha. Ninao uwezo. Ninao uwezo. Ninao uwezo, kama spika”

Kile kilichohofiwa, yaani viongozi kuingiza matakwa binafsi katika uendeshaji wa chombo cha umma, inaelekea ndio kinachotokea, maana Ndugai hakuficha hasira zake: “Huwezi kulitukana Bunge, unamtukana huyo spika halafu huyo huyo anakupa nafasi wewe uzungumze. Kwa sababu yeye ni malaika? Mimi ni binadamu mwenye damu na nyama, kama binadamu mwingine.” Sheria iliwekwa kudhibiti huu ubinadamu wa spika.

Spika aliendelea kuwaka: “Kwa hiyo kadri unavyoninyanyasa na kunidhalilisha mbele ya watu, na mimi nitatumia madaraka yangu na mamlaka niliyonayo ambayo nimepewa na nchi na nimepewa na Mungu kuona nini nifanye katika mamlaka niliyonayo.”

Kwa kasi tunayokwenda nayo ya watu kufanya wajisikiavyo sijui nini kitatokea mbele ya safari maana viongozi wote wana ubinadamu ambao kama haudhibitiwi, wadogo lazima wataumia maana viongozi watakuwa hawatabiriki.

Siasa za Albadiri zimerejea

Katika nchi nyingine zote, kukitokea tukio la uhalifu, vyombo vya dola hufanya uchunguzi hadi wanawang’amua wahalifu na kuwafikisha katika vyombo vya sheria au kuwaaadhibu kwa namna nyingine. Pia kukitokea jambo ambalo wananchi hawalipendi, huonesha hasira zao kwa kujitokeza kuandamana kulipinga jambo hilo.

Tanzania, hali ni tofauti kidogo. Tukio likiwa tata na gumu, na ikishindikana wahalifu kupatikana au mhalifu akijulikana lakini watu wakawa wanamuogopa, kuna silaha nyingine inaitwa Albadri, kisomo kinachosemekana kuwa ni cha Kiislamu cha kuadhibu wakora.

Hata hivyo, imani kubwa tuliyoiweka katika Albadiri ni kielelezo cha uvivu wetu wa kuhangaika kutatua matatizo yetu na badala yake kusukumizia matatizo yetu kwa ‘nguvu iliyo juu yetu.’ Nguvu iliyo juu inasaidia pale tu sisi wenyewe tukipambana na kutengeneza sababu ya kufikia tunayoyatarajia. Tunakwepa wajibu wetu.

Huko kulikotoka Uislamu, Saudi Arabia na nchi nyingine za Mashariki ya Kati ambako Mtume Muhammad na Maswahaba zake waliishi zaidi, umewahi kusikia kisomo hiki kinaitishwa kama njia ya kuwang’amua ‘wahalifu wasiojulikana’?

Lakini ninavyowajua Watanzania na muelekeo wa nchi yetu, naamini tutashuhudia Albadiri zaidi awamu hii.

Ni siasa mpya..

 Niliyoyataja hapo juu na mengine mengi tutakayoyashuhudia ni muelekeo wa siasa mpya za Tanzania. Miaka miwili tu katika miaka mitano ya kwanza ya awamu ya tano. Tumeona mengi. Kwa hali inavyoenda, huenda tukaona mengi zaidi. Tena ya kushangaza sana. Kwa sisi wanafunzi wa siasa, hiki ni kipindi cha kukaa macho muda wote, tukijifunza

No comments:

Post a Comment

Popular