Omog asikiliza vilio vya mashabiki wa Simba - KULUNZI FIKRA

Friday, 15 September 2017

Omog asikiliza vilio vya mashabiki wa Simba

 Mshambuliaji Laudit Mavugo huenda sasa akaanzia benchi katika michezo ijayo ya Simba ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ukiwamo wa Jumapili dhidi ya Mwadui FC, ili kutoa nafasi kwa kiungo Mohamed Ibrahim ‘Mo’ kuanza.

Kocha wa Simba, Joseph Omog, tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu amekuwa akimtumia Mo kama mchezaji wa akiba, huku akimpa nafasi ya kuanza Mavugo.

Mavugo, licha ya kupata nafasi hiyo, ameshindwa kuthibitisha ubora wake, baada ya kushindwa kupachika bao hata moja katika mechi mbili za Ligi Kuu ambazo Simba imecheza hadi sasa, na timu za Ruvu Shooting ilipoibuka na ushindi wa mabao 7-0 na Azam FC uliokwisha kwa suluhu.

Wakati Mavugo akipata bahati hiyo na kushindwa kuitumia, Mo licha ya kutokea benchi, amekuwa akionyesha kiwango maridadi, hatua iliyowafanya mashabiki wa Simba kuhoji sababu za kutopangwa katika kikosi kinachoanza.

Kilio cha mashabiki wa Simba kinaonekana kumfikia kocha wao, Omog, ambaye katika mazoezi ya timu hiyo jana kwenye Uwanja wa Uhuru, alionekana kumpanga Mo katika kikosi cha wachezaji 11 ambao wamekuwa wakianza katika michezo iliyopita.

No comments:

Post a Comment

Popular