KWA muda wa wiki tatu nimekuwa kimya katika safu hii. Kimekuwa kipindi cha hekaheka kwa nchi nzima kutokana na mambo yaliyotokea na ambayo yamewasumbua wengi. Miongoni mwa mambo hayo, mojawapo ni kupigwa risasi kwa Wakili Tundu Lissu akiwa bungeni Dodoma na kuumizwa vibaya kiasi cha watu wengi kuhofia maisha yake.
Napenda nilizungumzie hili, nikiwa pia na ombi maalumu kwa Mheshimiwa Rais John Magufuli (Itakumbukwa kwamba nilipoachia nilikuwa natoa maoni kuhusu jinsi Magufuli anavyoweza kujikinga na kiburi, kama yeye mwenyewe alivyoomba tumuombee asije akawa na kiburi).
Ni dhahiri kwamba aliyemshambulia (au waliomshambulia) Lissu walitaka kumuua. Ukali wa shambulio dhidi yake lilidhihirisha chuki nzito iliyokuwa mioyoni mwa watu waliofanya kitendo kile. Matumizi ya silaha za kivita na umiminaji wa risasi za idadi ile ni ishara kwamba kusudio lilikuwa kwamba Lissu asiondoke pale akiwa majeruhi bali aondoke akielekea chumba cha kuhifadhi maiti.
Waliosema wamesema waliyosema, na wala sina haja ya kuyarejea. Wapo waliotoa shutuma dhidi ya watu na dhidi ya asasi, na hizo pia sitaki kuzirejea. Ninachotaka kusema hapa, nikiomba kueleweka vyema, ni kwamba yeyote aliyemshambulia Lissu ni msaliti, mtu mwenye nia mbaya na nchi hii, mtu ambaye haitakii mema Tanzania.
Kwanza kabisa ningependa kusema kwamba katika historia yetu tumeweza kujiweka mbali kidogo na siasa za mauaji. Wenzetu katika nchi jirani na sisi wamekuwa na utamaduni wa kumaliza tofauti zao za kisiasa kwa mauaji ya wanasiasa. Hilo halijawasaidia sana kujenga nchi zenye amani, na hadi sasa wanahangaika kuitafuta amani ya kweli.
Nasi, iwapo tutakubali na tukaanza kuwamaliza wale tunaowaona kama maadui, tutakuwa tumejiingiza katika shimo ambalo litatumeza kabisa, tusiweze kutoka. Nchi zilizoingia huko zimepotea kabisa na huo ndio umekuwa mtindo wa kuendesha shughuli zao.
Kuua mpinzani wako au mtu ambaye unatofautiana naye kisiasa ni dalili kwamba umeshindwa katika mapambano ya hoja, kwamba hoja zake zimekushinda kuzijibu kwa hoja. Inapotokea aliyeshindwa kwa hoja anaona njia pekee ya kumnyamazisha mpinzani wake ni kumuua, inawezekana na wengine wakajihami kwa njia hizo hizo. Ikiisha kuwa mtindo ni ‘jino kwa jino’, nchi inakuwa imejiwashia moto ambao utaiangamiza.
Najua kwamba tunapenda sana kujitangaza kuwa ni nchi ya ‘amani na utulivu’. Lakini itatusaidia iwapo tutakumbuka alichotuambia Mwalimu Julius Nyerere miaka ya 1980, alipotukumbusha msemo wa Kiswahili, ‘Usione vinaelea, vimeumbwa.’ Aliongeza, ‘Kama amani huzuka hivi hivi bila kutengenezwa, kwa nini isizuke na kwingine?’
Ni nchi ya wendawazimu pekee inayoweza kuazimia kuwa na hali ya utovu wa amani. Nchi zote zinapenda amani, lakini nyingi hujikuta zimepoteza amani kwa sababu ya matendo ya watu wake, hasa watawala wake. Jukumu la kulinda na kuendeleza amani katika nchi ni jukumu la wananchi wake wote, lakini zaidi kuliko wote ni jukumu la watawala.
Waliomuumiza Lissu walitaka kupandikiza mbegu za kwanza za kuvunjilia mbali amani ya nchi hii, na inatakiwa sote tuwalaani kwa sauti zetu sote. Aidha, vyombo vya uchunguzi havina budi kufanya kila kinachowezekana kuwapata wahalifu hao na kuwafikisha mbele ya sheria. Si jambo linaloingia akilini kwamba risasi idadi ile zinaweza zikarindima mchana kweupe, mahali panapolindwa, halafu wahalifu wakaishia hewani kama majini.
Wapo watu waliopendekeza kwamba vyombo vya upelelezi vya mataifa makubwa kama FBI ya Marekani au New Scotland Yard vihusishwe iwapo tunaona kwamba vyombo vyetu havina uwezo wa kufanya kazi hiyo. Kama kila uchao tunakwenda kuomba misaada kutoka kwa mataifa haya, hata kwa mambo yasiyokuwa na maana, vipi tunapata kigugumizi katika kuomba msaada kwa jambo kubwa kama hili?
Aidha, kumekuwa na mikanganyiko isiyoelezeka miongoni mwa wakuu wa Bunge na serikali kuhusu matibabu ya Lissu. Inashangaza kuona jinsi baadhi yao wanavyojichanganya kiasi cha kuwafanya baadhi ya wanaohoji wajiulize maswali mengi, mojawapo likiwa hili: Je, kwa kuangalia jinsi wanavyolishughulikia suala la matibabu ya Lissu, watu hawa kweli walitaka Lissu apone?
Kutokana na matendo ya baadhi ya watu katika hali kama hii ya shambulio dhidi ya Lissu, mara nyingi mtu hahitaji kutamka neno lili kubainisha dhamira yake. Tendo moja la wema lililo wazi linafunika maneno elfu ya kumung’unyamung’unya. Lissu ameumizwa akiwa kazini, na alistahili kuhudumiwa kwa kila njia na waajiri wake.
Bahati njema ni kwamba kuvuta miguu kwa wakuu wa asasi hzio kumewasaidia wazalendo (wa ndani na wa nje) kwa kuwapa fursa ya kuonyesha mshikamano wao kwa kutoa michango binafsi. Inawezekana sasa Watanzania wamefikia kiwango kipya cha kudhihirisha mshikamano katika hali ngumu.
Ombi langu kwa Rais John Magufuli si kubwa. Kama nilivyosema huko nyuma, kama Rais wetu anahitaji kuepukana na kiburi anaweza kufanya hivyo bila kusubiri maombezi katika mahekalu. Ataepukana na kiburi iwapo atakubali kujishusha na kusikiliza wanayosema watu wake. Nilisema pia kwamba kusikiliza watu wako si kusikiliza tu yale yanayotamkwa, bali ni kusikiliza hata maneno ambayo bado hayajatamkwa.
Namuomba Rais Magufuli amtambue Tundu Lissu kama mzalendo, mpigania haki za wananchi wake wa kipindi kirefu. Kwamba Rais Magufuli ni mzalendo kwa jinsi anavyopambana dhidi ya dhuluma wanazofanyiwa Watanzania, haina maana kwamba hakuna wazalendo wengine. Lissu ni mmoja wao, miongoni mwa wale wasiosubiri kupata vyeo ili wawe wazalendo.
Lissu amekuwa msitari wa mbele katika kupigania maslahi ya nchi hii tangu miaka ya 1990, mimi nikiwa bado ndani ya chumba cha habari. Jina la Lissu na lile la Nshala Rugemeleza ni majina yaliyojitokeza kwa nguvu kubwa wakati ule wakiwa wanasheria wa LEAT, na tangu siku hizo Lissu amekuwa katika kila handaki la vita ya kuwakomboa Watanzania kiuchumi na kisiasa.
Kwamba anatofautiana na baadhi ya mitazamo ya Rais Magufuli si jambo linalomfanya kuwa msaliti. Niruhusuni kwa unyenyekevu mkubwa nitoe mfano wangu, japo sitaki kujiita mzalendo. Katika miaka hiyo hiyo ya 1990 nilipata msukosuko kutoka kwa wakuu wa serikali ya wakati huo, si kwa sababu nilikuwa mwizi ama mla-rushwa ama mhaini, bali kwa kuwaambia wakuu wa wakati ule kwamba wanasaidiana na waporaji wa nje kupora mali za wananchi wa nchi hii.
Mapambano haya ni yetu sote, na itakuwa ni jambo jema tukikubaliana kwamba hakuna mwenye ukiritimba wa uzalendo bali sote tunatakiwa tuchangie nguvu zetu kuiendeleza nchi yetu. Maneno ya mwisho ya Lissu bungeni dakika chache tu kabla hajamiminiwa risasi yawe ni maelezo maridhawa ya jinsi Lissu anavyojali maslahi ya nchi hii.
Iwapo Rais Magufuli ameweza kumtambua David Kafulila, ambaye alibandikwa jina la ‘Tumbili’ na wakuu wa serikali wa kipindi fulani, Magufuli anaweza sana kumtambua Lissu kama mtu aliyetoa mchango mkubwa kwa nchi hii.
Namuomba tena Rais Magufuli, tena namuomba kwa unyenyekevu mkuu, atambue kwamba anaambiwa uongo mwingi, na mambo mengine yamefichwa ili asiyaone. Aidha atambue kwamba watu wengi waliomzunguka ni waoga, waoga wakubwa ambao hawathubutu kumwambia jambo wasilokuwa na uhakika nalo kwamba litamfurahisha.
Akiendelea kuwategemea hawa kwa kila anachofanya, Rais Magufuli hataepuka kiburi hicho anachokichelea, bali atakijenga zaidi.
Thursday, 28 September 2017
Home
Unlabelled
Jenerali Ulimwengu: Rais Magufuli ataepukana na kiburi, ikiwa atakubali kujishusha
Jenerali Ulimwengu: Rais Magufuli ataepukana na kiburi, ikiwa atakubali kujishusha
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Popular
-
THIS ANNOUNCEMENT CONTAINS INSIDE INFORMATION Acacia Mining plc (“Acacia” or the “Company” or the “Group”) Management Changes Ac...
-
Tanzania’s Tunduru district is a major producer of gem-quality sapphire and ruby, along with exotic gems such as alexandrite and tsavor...
-
Moto mkubwa umelipuka na kuunguza soko la wafanyabiashara wadogo wadogo (machinga) katika eneo la Mbagala Rangi Tatu – Dar, asubuhi hii M...
-
Ofisi ya Spika wa Bunge imesema, mpaka sasa haijapokea barua toka kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini kupitia Chama cha...
-
Spika wa zamani, Pius Msekwa amesema Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu hakuwa analazimika kuandika barua kwa Spika wa Bunge...

No comments:
Post a Comment