SERIKALI imemuondoa nchini aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues, kwa madai ya kunyanyasa wafanyakazi wenzake aliokuwa akifanya nao kazi nchini.
Rodrigues anakuwa mwanadiplomasia wa pili kuondolewa nchini kwa maelekezo ya serikali baada ya Awa Dabo aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) naye kufanyiwa hivyo Aprili mwaka huu.
Tofauti na ilivyokuwa kwa Dabo, safari hii serikali kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa (UN) wametekeleza jambo hilo pasipo kutolewa kwa taarifa rasmi na pande zote ingawa inafahamika mwanamama huyo tayari ameondoka nchini takribani wiki tatu zilizopita.
“ Mimi si msemaji wa UN lakini naweza kukuthibitishia kwamba mama Rodrigues tayari ameondoka nchini takribani wiki tatu zilizopita na nafasi yake itajazwa baadaye na UNESCO baada ya kufanyika kwa mchakato wa kumtafuta mbadala. Sidhani kama UN wana mpango wa kutoa taarifa rasmi kuhusu hilo,” kulunzifikra blog imeambiwa na mojawapo ya vyanzo vyake ndani ya UN.
Kwa taratibu za kawaida, Serikali ya Tanzania haiwezi kumfukuza mtumishi wa UN moja kwa moja, isipokuwa ni lazima itoe hoja zake kwa taasisi hiyo na baada ya kuwa kuna ushahidi wa tuhuma zilizopo, mfanyakazi huweza kuondolewa. Kutokana na utaratibu huu, UN ndiyo humuondoa mtumishi wake kwenye nchi husika lakini kiufundi ni serikali ndiyo inakuwa imemuondoa.
Katika siku za karibuni, kulikuwa na minong’ono katika duru za kibalozi nchini kwamba Rodrigues ambaye ni raia wa Angola alikuwa ameondolewa kwa sababu ya upinzani wake dhidi ya mpango wa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli kufufua mradi wa kufua umeme kwa kutumia nishati ya maji wa Stiegler’s Gorge.
Mradi huo utajengwa ndani ya eneo la Hifadhi ya Selous ambayo tayari UN kupitia UNESCO umeitangaza kuwa ni mojawapo ya maeneo yanayotakiwa kutunzwa duniani kutokana na umuhimu wake katika dhana nzima ya uhifadhi wa mazingira duniani.
Hata hivyo, uchunguzi wa kulunzifikra blog umebaini kwamba kulikuwa na tuhuma mbalimbali za kunyanyasa wafanyakazi wa UNESCO wanaofanya kazi nchini dhidi ya raia huyo wa Angola na hizo ndiyo zilikuwa hoja kuu za serikali ya Tanzania kwenye kutaka Rodrigues aondolewe nchini.
Juhudi za kumpata Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Augustine Mahiga, kuzungumzia taarifa hizi wala wasaidizi wake hazikuzaa matunda kwa maelezo kuwa walikuwa wamekwenda nchini Marekani kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) uliokuwa ukifanyika jijini New York, Marekani.
Kulunzifikra blog haikuweza pia kumpata Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, ambaye alielezwa kuwa kwenye msiba wa kufiwa na mmoja wa ndugu zake wa karibu mwishoni mwa wiki iliyopita.
Hata hivyo, mmoja wa maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ambaye hakutaka kunukuliwa katika habari hii, alikiri kwamba Rodrigues tayari ameondoka nchini na kwamba tatizo ni unyanyasaji wake wa wafanyakazi na si sababu nyingine.
“ Ngoja nikusaidie rafiki yangu usije ukaandika mambo ambayo watu wanaowajua watawashangaa. Hakuna mambo ya Stiegler wala nini, ni masuala ya uhusiano wake na wafanyakazi wake tu. Kwa bahati mbaya huwezi kujua majina ya watu walionyanyaswa na mama huyo kwa sababu taarifa zao wakitoa wanataka wawe anonymous (wasitajwe). Ushahidi wote wa vitendo vyake upo na ndiyo maana UNESCO wamekubali kumuondoa,” alisema ofisa huyo mwandamizi.
Kwa mujibu wa wasifu rasmi wa Rodrigues uliopo kwenye tovuti ya UNESCO, mwanamama huyo alipata elimu yake ya sekondari nchini Ureno na ana elimu ya shahada ya uzamili aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Nijmegen nchini Uholanzi. Mwanamama huyo ameelezwa kuwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika masuala ya kupanga na kutekeleza sera za kielimu na alijiunga na UN mwaka 1996.
Dabo na Rodrigues wote ni wanawake na wameondoka nchini kwa makosa yanayofanana na Raia Mwema linafahamu kwamba wafanyakazi wa ngazi za chini wa UN wamefurahishwa na hatua zilizochukuliwa lakini mabosi wao sasa wameelezwa kuwa katika hali ya ‘matumbo joto’.
“ Ninachofahamu ni kwamba wafanyakazi wa kada ya chini wamefurahishwa na hatua za serikali kwa sababu unyanyasaji wa huyo mama ulikuwa unajulikana ingawa hatua zilikuwa hazichukuliwi. Watu waliokosa sasa ni mabosi wao kwa sababu sasa wanajua kosa lolote wanaweza kujikuta nao wakipatwa na yaliyowakuta wenzao,” gazeti hili limeambiwa.
Katika taarifa rasmi ya serikali iliyotolewa na serikali Aprili 25 mwaka baada ya kumfukuza Dabo, mwanadiplomasia huyo alielezwa pia kutokuwa na uhusiano mzuri na wafanyakazi wenzake –ingawa kulikuwa na taarifa nyingine kinzani katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
Taarifa ya serikali iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje wakati huo ilisema; “Serikali ilifikia uamuzi huo kutokana na Dabo kutokuwa na maelewano mazuri na baadhi ya watumishi wenzake na menejimenti ya shirika hilo, hivyo kupelekea kuzoretesha utendaji wa shirika hilo nchini na kupunguza kasi ya kuleta maendeleo kwa Watanzania endapo hatua za haraka zisingechukuliwa.
“Baada ya kuthibitishiwa kuondoka nchini, serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje imetoa rai kwa UNDP kuwakumbusha watumishi wake kuwa kipaumbele chao ni kufanya kazi na serikali ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano na Malengo ya Maendeleo Endelevu ambayo yamefafanuliwa katika Agenda ya Mwaka 2030”.
Friday, 29 September 2017
Home
Unlabelled
Balozi mwingine afukuzwa Tanzania
Balozi mwingine afukuzwa Tanzania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Popular
-
THIS ANNOUNCEMENT CONTAINS INSIDE INFORMATION Acacia Mining plc (“Acacia” or the “Company” or the “Group”) Management Changes Ac...
-
Tanzania’s Tunduru district is a major producer of gem-quality sapphire and ruby, along with exotic gems such as alexandrite and tsavor...
-
Moto mkubwa umelipuka na kuunguza soko la wafanyabiashara wadogo wadogo (machinga) katika eneo la Mbagala Rangi Tatu – Dar, asubuhi hii M...
-
Ofisi ya Spika wa Bunge imesema, mpaka sasa haijapokea barua toka kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini kupitia Chama cha...
-
Spika wa zamani, Pius Msekwa amesema Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu hakuwa analazimika kuandika barua kwa Spika wa Bunge...

No comments:
Post a Comment