Serikali yasitisha usajili wa NGO's - KULUNZI FIKRA

Tuesday 22 August 2017

Serikali yasitisha usajili wa NGO's


Serikali imetangaza usitishaji wa usajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) kuanzia Agosti 21 hadi Novemba 30, mwaka huu ili kufanya uhakiki wa NGO’s zilizosajiliwa.

Hatua hiyo imetangazwa jana na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Sihaba Nkinga, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari.

“Napenda pia kuujulisha umma kuwa kuanzia Agosti 21, 2017 hadi Novemba 30, 2017 usajili wa NGO’S mpya utasimamishwa, ili kutoa fursa kwa wataalamu kuchakata taarifa kutoka kwenye vituo vingine kuhakiki NGO’s zilizosajiliwa,”amesema Nkinga.

Bw. Nkinga amesema baada ya uhakiki huo unaotarajia kufanyika nchi nzima kukamilika, NGO’s zote ambazo hazitakuwa zimefanyiwa uhakiki zitafutwa kwenye Rejista na hazitaruhusiwa kuendesha shughuli zao nchini.

“Wakati tunaendelea na zoezi la uhakiki tutafanya tathmini ya mwenendo wa uhakiki katika kanda zote nchini na hatimaye kutoa uamuzi stahiki, ili kuhakikisha kuwa zoezi hili linafanikiwa na wadau wetu wanahudumiwa kwa ufanisi mkubwa,”amesema Nkinga huku akiwakumbusha wahusika wa NGO’s kuwasilisha vyeti vyao vya usajili mapema kwa njia ya mtandao.

“Niwakumbushe pia, kuwa ni vema kuzingatia kuwa wakati wa uhakiki kila NGO’s inatakiwa kuwasilisha cheti halisi cha usajili na nakala ya cheti hicho, NGO-Fomu/UHK/2017 iliyojazwa vizuri. Fomu hii inapatikana katika tovuti ya uratibu wa NGOs kwa anuani ya www.tnnc.go.tz, stakabadhi za malipo ya ada ya mwaka au hati ya malipo benki toka kusajiliwa kwa shirika, Barua kutoka kwa ofisa maendeleo ya jamii (Mkoa/ wilaya/halmashauri au Manispaa) ikithibitisha uwapo wa ofisi ya shirika na nakala ya katiba ya NGO iliyothibitishwa na msajili wa NGOs,” amesema Nkinga.

Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiserikali nchini Tanzania, Nicholaus Zacharia, amewatoa hofu wamiliki wa mashirika hayo na kuwataka kila mmoja kushiriki katika uhakiki huo.

“Sisi kama viongozi wenu tumejilidhisha serikali haina mpango wowote mbaya na Azaki zetu, hivyo mtu atakayekwambia usishiriki katika uhakiki anakutakia uende jehanamu,”amesema Zacharia.

Hata hivyo, Zacharia ameiomba serikali kuona ni jinsi gani inaweza kuanzisha bodi itakayokuwa inasimamia mashirika hayo tofauti na baraza hilo ambalo limekuwa likidumu kwa miaka mitatu.

No comments:

Post a Comment

Popular