Dar kinara wa matusi,Mwanza wizi - KULUNZI FIKRA

Thursday 24 August 2017

Dar kinara wa matusi,Mwanza wizi

 
 Dar es Salaam. Imebainika kwamba pamoja na uwepo wa sheria ya makosa ya mtandao lugha ya matusi imeendelea kutumika huku mkoa wa Dar es Salaam ukiwa kinara.

Pia Mkoa wa Mwanza nao umebainika kuwa kinara kwa upande wa makosa ya wizi fedha mtandaoni ukilinganisha na mikoa mingine.

Takwimu zilizotolewa na jeshi la polisi zimeonyesha kuwa jumla ya matukio 327 ya matusi mtandaoni yameripotiwa kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu.

Msemaji wa Jeshi hilo ACP Barnaba Mwakalukwa amesema matukio mengi ya makosa ya matusi yanatokea wilaya ya Temeke.

Hata hivyo Mwakalukwa amesema takwimu hizo inaonyesha kupungua ikilinganishwa na mwaka jana ambapo matukio kama hayo 911 yaliripotiwa na wilaya ya Kinondoni iliongoza.

"Jumla ya matukio 1663 ya wizi wa fedha kwa njia ya mtandao zimeripotiwa huku mkoa wa Mwanza ukionekana kuwa kinara ikifuatiwa na Ilala na Kinondoni.

"Unaweza kuuliza kwa nini Mwanza, ule mji umekua kuna wafanyabiashara wakubwa, wahalifu nao wanabuni mbinu mpya," amesema

Amesema jumla ya watuhumiwa 315 walikamatwa kuhusiana na makosa ya uhalifu mtandaoni na kesi 153 zimefikishwa mahakamani.

Kati ya kesi hizo wahusika katika kesi 19 walikutwa na hatia na nyingine zipo chini ya upelelezi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Hamza Hassan amesema ipo haja ya kuendelewa kutolewa elimu kuhusu sheria ya mtandao ili kupunguza vitendo vya ukiukwaji maadili.

"Unaweza kufanya jambo leo mtandaoni halafu athari zake zikaanza kuonekana baada ya miaka kadhaa, tuitumie vyema mitandao na elimu zaidi itolewe,"

Hassan akiwa na kamati yake wametembelea Mamlaka ya Mawasiliano TCRA na kupewa semina kuhusu sheria ya makosa ya mtandao.

No comments:

Post a Comment

Popular