Kijana mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Sadiki, ambaye ni muuza mishikaki katika eneo lililo karibu na jengo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar esalam anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kudaiwa kuwa anauza mishkaki ya nyama za paka.
Walaji wengi wa mishkaki ya Sadiki walikuwa wakipatwa na mashaka kuhusu nyama hiyo kutokana na ladha yake kuwa tofauti, lakini kila alipomuuliza kuhusu jambo hilo, jamaa huyo alikuwa akiwatoa hofu kwa kuwaambia kuwa ni nyama ya ng’ombe.
Imedaiwa kuwa kutokana na hofu ya wateja wa mishkaki hiyo kuongezeka, wananchi wa eneo hilo waliamua kumuwekea mtego ili kubaini ukweli.
Alhamisi iliyopita, wakati akiwasili katika kijiwe chake kuendelea na kazi yake ya kuuza mishikaki, ghafla wananchi walimvamia na kumnyang’anya ndoo yake ya nyama na kuifungua, ndipo zilipokutwa nyama hizo zilizodaiwa kuwa za paka.
Wananchi wenye jazba baada ya kuona hivyo walitaka kumuangushia kipigo, lakini walitokea polisi wa doria ambao walimuokoa mfanyabiashara huyo na kwenda naye kituoni kumhoji zaidi kuhusiana na tuhuma hizo.

No comments:
Post a Comment