Lissu apata dhamana kwa shariti la kubaki Dar - KULUNZI FIKRA

Thursday, 27 July 2017

Lissu apata dhamana kwa shariti la kubaki Dar

Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu ameachiwa kwa dhamana na mahakama ya hakimu mkazi Kisutu baada ya kutupilia mbali pingamizi la serikali la kupinga asipewe dhamana hiyo.

Mahakama hiyo chini ya Hakimu mkazi mkuu, Wilbard Mashauri imefikia uamuzi huo baada ya kusikiliza hoja za pande zote, kufuatia maombi ya dhamana yaliyowasilishwa na upande wa utetezi wenye jopo la mawakili 18 wakiongozwa na Fatma Karume pamoja na Peter Kibatala.

Licha ya kumuachia kwa dhamana yenye masharti ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya shilingi milioni 10 kila mmoja, pia mahakama imetoa sharti la kumtaka Lissu kutosafiri nje ya Dar es Salaam.

Lissu alisomewa shtaka moja la kutoa matamshi ya uchochezi Julai 24, mwaka huu baada ya kukamatwa siku ya Alhamisi wiki iliyopita na kuwekwa chini ya uangalizi wa jeshi la polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam.

Mbunge huyo wa Singida Mashariki alinyimwa dhamana kutokana na upelelezi kutokamilika baada ya kuwepo kwa pingamizi la upande wa jamhuri  uliodai kuwa mshtakiwa hastahili kupata dhamana kwa madai kuwa amekuwa akirudia makosa ya aina hiyo mara kwa mara.

No comments:

Post a Comment

Popular